BRAZIL

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis atoa onyo kwa mataifa yanayohalalisha matumizi ya mihadarati

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akiwa katika Mji wa Aparecida akihutubia Vijana Wakatoliki
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akiwa katika Mji wa Aparecida akihutubia Vijana Wakatoliki REUTERS/Paulo Whitaker

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa onyo kwa mataifa ya Latin Amerika kuacha mara moja hatua yake ya kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya sanjari na kuendelea kubariki matumizi ya sera za kiliberali zinazochangia kutambulika kwa ndoa za jinsia moja.

Matangazo ya kibiashara

Papa Francis ambaye ni mzaliwa wa Argentina akiwa ziarani nchini Brazil amesema hatua hiyo ya kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kushabikia uwepo wa sera za kiliberali havitasaidia kwa namna yoyote ile kupunguza matatizo yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Latin Amerika.

Kauli ya Papa Francis kukemea uhalalishwaji wa matumizi ya dawa za kulevya imeitoa alipopata nafasi ya kuwatembelea waathiriwa wa matumizi ya dawa hizo waliokuwa wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospital ya Mtakatifu Francis huko Jijini Rio De Janeiro.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani amesema matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa ni chachu ya kutokea kwa vifo vya vijana wengi na hata kupotea kwa nguvu kazi ya mataifa mbalimbali kwa kuwa waathirika wengi wamekuwa ni vijana.

Papa Francis ametoa tamko hilo mbele ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya katika Hospital ya Mtakatifu Francis huku mvua kubwa ikinyesha wakati alipowasili kukutana na watu hao ambao wamekuwa wakitumia mihadarati.

Tamko la Papa Francis limekuja huku Rais wa Uruguay Jose Mujica akipendekeza Taifa hilo lihalalishe matumizi ya mihadarati hasa marijuana ambayo nayo yamekuwa yakipingwa kwa kiwango kikubwa.

Mataifa ya Amerika Kaskazini na Kusini yameendelea kukabiliwa na tatizo la uwepo wa biashara na magenge ya wauzaji wa dawa za kulevya kitu ambacho kimechangia watu wengi kupoteza maisha.

Mexico imeshuhudia zaidi ya watu 70,000 wakipoteza maisha tangu mwaka 2006 kutokana na biashara za dawa za kulevya lichas ya kwanza Serikali imeendelea kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kuyamaliza magenge yanayofanya shughuli hizo.