MAREKANI-URUSI

Marekani imetoa ombi jingine kwa Urusi iwakabidhi Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi la CIA Edward Snowden

Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi nchini Marekani CIA Edward Snowden amepata nyaraka za kumuwezesha kuondoka Uwanja wa Ndege nchini Urusi
Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi nchini Marekani CIA Edward Snowden amepata nyaraka za kumuwezesha kuondoka Uwanja wa Ndege nchini Urusi Reuters

Marekani imerudia tena ombi lake kwa Urusi ikiitaka serikali ya nchi hiyo kumkabidhi kwenye vyombo vya sheria Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi la CIA Edward Snowden ili aweze kukabiliana na mashtaka yanayomkabili ya kuvujisha siri za Shirika hilo.

Matangazo ya kibiashara

Ombi la Marekani linakuja baada ya Urusi kumkabidhi nyaraka zinazomwezesha Snowden kutoka katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Sheremetyevo alipokuwa anakaa kwenye eneo la abiria wanaopita nchini humo akitokea nchini China kwa kuwa hakuwa na kibali cha kumruhusu kuingia katika Taifa hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ametoa ombi akiliekeleza kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov akitaka Moscow wamkamate Snowden na kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria vya Washington.

Snowden kwa kipindi cha majuma manne amekuwa akiishi kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa Moscow unaotambulika kwa jina la Sheremetyevo kwa kuwa hakuwa na nyaraka zinazomruhusu kuingia katika nchi hiyo lakini sasa amepata ruhusa hiyo baada ya taratibu zake kukamilika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Jen Psaki amesema wanamatumaini ombi lao litafanyiwa kazi na Serikali ya Moscow ili Snowden arudishwe Washington na akabiliane na sheria kutokana na makosa ambayo ameyatenda.

Psaki amekiri licha ya kupata taarifa za Snowden kuweoa nyaraka zinazomwezesha kuondoka katika Uwanja wa ndege na hata kuomba hifadhi nchini Urusi lakini wanamatumaini Serikali ya Moscow itafanyiakazi ombi lao.

Mapema Msemaji wa ikulu ya Marekani maarufu kama White House Jay Carney amesema wameomba wapatiwe maelezo zaidi kutoka kwa Serikali ya Moscow ili kujua hadhi ambayo amepewa baada ya kupata nyaraka hizo za awali.

Carney amesisitiza msimamo wa nchi hiyo ni kuhakikisha Snowden anafikishwa kwenye vyombo vya usalama kujibu makosa yanayomkabili ya kuvujisha siri za Shirika la Kijasusi la CIA.

Edward Snowden aliingia nchini Urusi tarehe 23 mwezi Juni akitokea China ambako alikuwa anapata hifadhi ikiwa ni harakati zake za kuhakikisha anapata hifadhi baada ya kutoa siri za CIA kubainisha imekuwa ikirekodi mawasiliano ya simu za wananchi.