MAREKANI-MISRI

Serikali ya Marekani yatangaza mpango wa kuchelewesha msaada wake wa Ndege za Kijeshi wa Misri kutokana na uwepo wa machafuko

Ndege za Kijeshi aina ya F-16 ambazo Marekani inatarajia kuipa Serikali ya Misri
Ndege za Kijeshi aina ya F-16 ambazo Marekani inatarajia kuipa Serikali ya Misri

Serikali ya Marekani imetangaza mpango wake wa kuchelewesha kutoa msaada wa ndege za kijeshi aina ya F-16 kwa serikali ya Misri kutokana na kuendelea kwa machafuko nchini humo tangu kuangushwa kwa Mohamed Morsi ambao wafuasi wake wamekuwa mstari wa mbele kuandaa maandamano kila uchao.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Ulinzi ya Marekani maarufu kama Pentagon ndiyo imetangaza uamuzi wa kuchelewesha msaada huo wa ndege za kijeshi kwa Serikali ya Cairo ikisema hali ya kutetereka kwa usalama imechangia kufikiwa kwa uamuzi huo.

Msemaji wa Pentagon George Little akizungumza na waandishi wa habari amesema bado wataendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Serikali ya Misri kutokana na uhusiano baina ya mataifa hjayo kuwa ni wa kihistoria.

Little amesisitiza msaada huo wa ndege za kijeshi utakabidhiwa kwa Misri kama ulivyopangwa lakini hadi pale ambapo watajiridhisha hali ya usalama imeimarika ili kusaidia juhudi za ulinzi wa taifa hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alishampigia simu Mkuu wa majeshi ya Misri Jenerali Abdel Fattah Al Sisi kumueleza uamuzi wa serikali yake kuchelewesha ufadhili wao wa ndege hizo za kijeshi.

Little amesema mazungumzo hayo baina ya Waziri Chuck na Jenerali Al Sisi yalikuwa ni ya manufaa ambapo pande zote mbili zilielewana juu ya sababu ambazo zimechangia kuchukuliwa kwa hatua hiyo bila ya kutoa maelezo zaidi.

Msemaji huyo wa Pentagon hakueleza kwa kina ni kwa nini Rais Barack Hussein Obama amechukua uamuzi huo wa kuchelewa kutoa msaada huo wa ndege za kijeshi zaidi ya kutaja tu hali ya usalama.

Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Msemaji wake Jen Psaki naye amesisitiza kuchukuliwa kwa uamuzi huo wa kucheleweshwa kutolewa kwa ndege hizo za kivita aina ya F-16 bila ya kusema kwa kina kilichochangia kuchukuliwa uamuzi huo.

Misri kwa sasa imekuwa ikishuhudia maandamano yanayofanywa na wafuasi wa Mohamed Morsi aliyeondolewa madarakani na Jeshi huku wao wakipinga uwepo wa Serikali ya Mpito inayongozwa na Adly Mahmud Mansour.

Wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood amejiapiza kuendelea na maandamano yao licha ya Jenerali Al Sisi kuruhusu kufanyika kwa maandamano ya kitaifa siku ya Ijumaa ili kutoa ruhusa kwa Jeshi kuweza kukabiliana na machafuko pamoja na vitendo vya kigaidi.