JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO

Waasi wa Kundi la M23 wajigamba kuwaua Wanajeshi wa FARDC 400 kwenye mapigano yaliyodumu kwa Siku 10

Msemaji wa Kijeshi wa Kundi la Waasi la M23 Vianney Kazarama ambaye ametangaza vifo vya Wanajeshi wa FARDC
Msemaji wa Kijeshi wa Kundi la Waasi la M23 Vianney Kazarama ambaye ametangaza vifo vya Wanajeshi wa FARDC

Kundi la Waasi la M23 ambalo linapambana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC limeibuka na kujigamba kuwaua wanajeshi zaidi ya mia nne wa Jeshi la Serikali la FARDC kwenye mapambano yaliyodumu kwa siku 10.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Kijeshi wa Kundi la Waasi la M23 Kanali Vianney Kazarama amesema wamewaua wanajeshi hao pamoja na kuwajeruhi wengine ambao idadi yao bado hawajaijua.

Kanali Kazarama amekiri pia wapiganaji wao sita wameuawa na wengine kumi na wanne wakijeruhiwa kutokana na mapigano hayo yaliyokuwa yanaendelea karibu kabisa na Mji wa Goma.

Taarifa hizi zinakuja baada ya hapo awali Jeshi la FARDC kuweka bayana liliwaua Waasi mia moja ishirini kutoka Kundi la M23 huku wenyewe wakipoteza wanajeshi wao kumi kwenye uwanja wa mapambano.

Kanali Kazarama ametoa kauli hiyo kipindi hiki mapigano mapya yakizuka tena siku ya jumatano baina ya Waasi wa M23 na Jeshi la FARDC lengo la waasi likiwa ni kuchukua Mji wa Goma ambao umekuwa ukilindwa vikali.

Msemaji huyo wa Kijeshi wa Kundi la Waasi la M23 amekiri wapiganaji wao kuanza kujibu mashambulizi yaliyokuwa yamefanywa na Jeshi la FARDC waliokuwa wanatumia helkopta za kijeshi kulenga ngome zao.

Mapigano hayo yameonekana yakichacha katika Mji wa Kanyaruchinya uliopo kilometa 12 kutoka Mji wa Goma ambapo Jeshi la FARDC imeshusha mabomu katika maeneo yote ambayo yanakaliwa na Waasi wa M23.

Kanali Kazarama hakuacha kukiri mashambulizi hayo yamechangia madhara makubwa kwa wananchi ambao wengi wao wamelazimika kukimbilia Mji wa Goma na hata wengine wakiomba hifadhi katika mataifa jirani.

Jeshi la Serikali la FARDC limeendela kusisitiza limefanikiwa kuzima kabisa mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Kundi la Waasi la M23 kipindi hiki Wanajeshi wa Kikosi Maalum cha Umoja wa Mataifa UN kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini wakiwa Mashariki mwa DRC.