UHISPANIA

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy atangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuwakumbuka watu 78 waliopoteza maisha kwenye ajali ya Garimoshi

Mabehewa ya garimoshi lililopata ajali nchini Uhispani katika Jiji la Compostelle na kusababisha vifo vya watu 77
Mabehewa ya garimoshi lililopata ajali nchini Uhispani katika Jiji la Compostelle na kusababisha vifo vya watu 77 REUTERS/Oscar Corral

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametangaza siku tatu za maombolezi nchini mwake kwa lengo la kuwakumbuka watu sabini na nane waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari moja iliyotokea karibu na Jiji analoishi la Santiago de Compostela. Rajoy alipata nafasi ya kufika eneo ilipotokea ajali hiyo na kisha kuwatembele Hospital majeruhi ambao wanaendelea kupatiwa matibabu wanaotajwa kufikia zaidi ya mia moja na arobaini na wanne. Waziri Mkuu Rajoy licha ya kutangaza siku hizo tatu za maombolezo ya kitaifa lakini pia ametaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kutokea kwa ajali hiyo ya garimoshi.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu zinaonesha watu sabini na nane wamepoteza maisha na wengine zaidi ya mia moja na arobaini wamejeruhiwa baada ya kutokea ajali hiyo iliyosababishwa na kutoka kwenye njia yake kitu kinachotajwa kuchangiwa na mwendo kasi.

Taarifa zinasema miili ya watu sabini na watatu ilipatikana eneo la ajali huku watu wengine watano wakifikwa na umauti wakiwa wamefikishwa hospital kuanza kupatiwa matibabu baada ya kujerujhiwa.

Duru za Kitabibu zinasema huenda idadi ya watu watakaopoteza maisha ikaongezeka kutokana na wengi wa wamajeruhiwa kuwa katika hali mbaya kutokana na kupata majeraha makubwa.

Ajali hiyo imetokea katika Mkoa wa Galicia uliopo jirani na Jiji la Santiago de Compostela ambapo garimoshi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 218 wakati linapata ajali hiyo inayoelezwa imechangiwa na uzembe wa nahodha wake.

Mabehewa yote nane ya garimoshi hilo yalitoka kwenye njia yake kabla ya mabehewa manne hayajapinduka juu chini na kufuatiwa na moshi mkubwa uliozingira eneo hilo kabla ya watu wengine kurushwa nje.

Vyombo vya Habari nchini Uhispania zimeripoti chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambao ulikuwa ni mara mbili ya ule ambao ulikuwa unapaswa kutumika na nahodha wa garimoshi hiyo.

Mamlaka nchini Uhispania hazijazungumza chochote kama chanzo cha kutokea kwa ajali hiyo inayotajwa kuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka arobaini ya taifa hilo na tayari uchunguzi umeanza.

Kikosi cha Uokoaji kinaendelea na jukumu la kuangalia iwapo kuna miili yoyote imesalia ndani ya mabaki ya mabehewa hayo kipindi hiki juhudi za kuyaondoa ikitarajiwa kuanza wakati wowote na kusafisha eneo hilo.

Mashuhuda wa ajali hiyo wamekiri garimoshi hilo lilikuwa kwenye mwendo mkali zaidi kitu ambacho kinaweza kikawa sababu ya kutokea kwake na wametaka uchunguzi ufanyike haraka kubaini chanzo halisi.

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametembelea eneo la ajali na kuangalia madhara yaliyotokea kipindi hiki Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akitoa wito wa kuwaombea majeruhi.