SYRIA-UMOJA WA MATAIFA

Takwimu za Umoja wa Mataifa UN zaonesha watu zaidi ya 100,000 wamepoteza maisha nchini Syria katika miezi 28 ya machafuko

Mapigano yanayoendelea nchini Syria yamechangia vifo vya watu zaidi ya 100,000 tangu kuanza kwake miezi 28 iliyopita
Mapigano yanayoendelea nchini Syria yamechangia vifo vya watu zaidi ya 100,000 tangu kuanza kwake miezi 28 iliyopita REUTERS/Khalil Ashawi

Umoja wa Mataifa UN umetoa takwimu zinazoonesha watu zaidi ya 100,000 wamepoteza maisha nchini Syria tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Wapinzani na Jeshi linalomtii Rais Bashar Al Assad yaliyodumu kwa zaidi ya miezi ishirini na nane sasa.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amesema watu zaidi ya laki moja wamepoteza huku wengine mamilioni wakilazimika kuyakimbia makazi yao wakijiepusha na madhara ya vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.

Ban amekiri ongezeko hilo la vifo limeendelea kuleta hofu juu ya hali ya usalama wa baadaye wa Syria kutokana na mapigano baina ya Wapiganaji wa Wapinzani na Jeshi la Serikali ya Damascus kuendelea kushika kasi.

Katibu Mkuu wa UN amesisitiza mapigano hayo yamechangia mzigo wa wakimbizi kwa mataifa jirani ambayo yamelazimika kuendelea kupokea watu hao wanaokimbia machafuko kwa sasa.

Ban ametoa wito kwa Marekani na Urusi kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana ili mazungumzo ya Geneva yafanyike na kuzileta pamoja pande zinazohasimiana nchini humo kwa zaidi ya miaka miwili.

Katibu Mkuu Ban amesisitiza mazungumzo ndiyo njia pekee ambayo inaweza ikasaidia kupatika kwa suluhu nchini Syria na hatimaye vita vya wenyewe kwa wenyewe vikamalizwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema wanafanya kila linalowezekana wakishirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov kuhakikisha mazungumzo ya Geneva yanafanyika.

Kerry ameweka bayana lengo lao ni kuhakikisha Serikali ya Damascus na Wapinzani wanafika kwenye meza ya mazungumzo huko Geneva ili kusaka suluhu ya kudumu ya machafuko hayo.

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Baraza la Upinzani nchini Syria SNC Ahmad Jarba ametoa wito kwa Marekani kuwapatia msaada wa kijeshi ili waweze kuendelea na mapigano dhidi ya Jeshi la Serikali.

jarba ametoa kauli hiyo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Kerry na kumueleza wanahitaji msaada wa haraka wa silaha kitu ambacho kitawasaidia kusonga mbele kwenye mapigano hayo.

Haya yanakuja kipindi hiki mapigano makali yakiendelea kushuhudiwa katika Mji wa Homs ambao unashikiliwa na Wapinzani huku Jeshi la Rais Assad likihaha kuhakikisha linaukomboa.