MISRI-UN

Ban Ki Moon aitahadharisha serikali ya mpito ya Misri

REUTERS/Khaled Abdullah

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ameitaadharisha Serikali ya mpito kuwa mauaji ya waandamanaji nchini humo yanatatiza juhudi za kuinusuru nchi hiyo na mgogoro unaoendelea hivi sasa. Ban alizungumza na Waziri Mkuu Mohamed El Baradei na Mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki na Qatar na Mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu juu ya hali inavyoendelea hivi sasa nchini Misri.

Matangazo ya kibiashara

Katika mazungumzo na El Baradei, Ban amerejea wito kutaka kuachiwa huru kwa aliyekuwa Rais wa Misri, Mohamed Morsi au kumfungulia mashtaka kwa uwazi kabisa.

Katika hatua nyingine Baraza la Ulinzi nchini humo limewaonya wafuasi wa Morsi kuwa Jeshi litachukua hatua madhubuti ikiwa Waandamanaji watatumia vibaya haki yao ya kuandamana kwa amani na kuwa watachuuliwa hatua ikiwa watavunja sheria.

Licha ya onyo hilo ghasia zimeendelea kushuhudiwa na wafuasi wa Morsi wameapa kuendeleza harakati zao mpaka pale kiongozi wao atakaporejeshwa madarakani.

Vikosi vya usalama vinashutumiwa kutumia silaha nzito dhidi ya waandamanaji, taarifa ambazo zimeendelea kukanushwa na wizara ya mambo ya ndani ambao wanadai wamekuwa wakitumia mabomu ya kutoa machozi pekee katika kuwatawanya waandamanaji.