ISRAELI-PALESTINA-MAREKANI

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yarejea

Reuters

Maafisa wa Israeli na Palestina wanaanza mazungumzo ya amani huku Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa na matumaini kuwa jitihada zake za kidiplomasia zitazaa matunda ya kusaka amani eneo la Mashariki ya Kati.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe wa pande zote mbili wataandaa mpango juu ya namna ambayo mazungumzo hayo yatafanyika, Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Jen Psaki ameeleza.

Ndoto za kufikiwa amani katika mashariki ya kati kwa miongo kadhaa zimekuwa zikitiliwa juhudi na Marekani lakini ziligonga mwamba tangu mwezi Septemba mwaka 2010.

Mjumbe wa Israel katika mazungumzo hayo ni Waziri wa Sheria Tzipi Livni na Mwakilishi wa Palestina ni Saeb Erekat.

Mazungumzo ya awali yanafanyika jumatatu hii na jumanne jijini Washington nchini Marekani, huku viongozi wa pande zote wakielezwa kuwa tayari kufanya maamuzi magumu katika kuelekea kupatikana amani.

Mazungumzo hayo yameanza saa kadhaa baraza la Mawaziri la Israel kuidhinisha pendekezo la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu la kuwaachia huru wafungwa 104 wa Kipalestina waliokuwa wanashikiliwa.

Mwishoni mwa juma Isarel pia ilipitisha muswada wa sheria utakaowawezesha raia wake kupigia kura ya maoni kila makubaliano ya amani yatakayofikiwa kati yake na Palestina, sheria ambayo imetajwa kama mojawapo ya jitihada za kuwashirikisha wananchi katika kila maamuzi muhimu kuhusu historia ya nchi hiyo.