MALI

Zoezi la kuhesabu kura za urais wa Mali laendelea kwa amani

REUTERS/Joe Penney

Zoezi la kuhesabu Kura nchini Mali limeendelea baada ya kutamatika kwa upigaji kura za Uraisi. Mamilioni ya wananchi walijitokeza kushiriki zoezi hilo siku ya jumapili na kutupilia mbali vitisho vya uvunjifu wa amani vilivyotolewa na kundi la wapiganaji wa eneo la kaskazini mwa nchi hiyo MUJAO.

Matangazo ya kibiashara

Waangalizi wa kimataifa wamesifu idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza huku kukiwa na ulinzi mkali katika vituo mbali mbali nchini humo, kuanzia katika mji mkuu Bamako.

Mpaka asubuhi ya jumatatu hakukuwa na uvunjifu wa amani ulioripotiwa kujitokeza dhidi ya wapiga kura wala wasimamizi wa zoezi hilo.

Raia wa Mali walitakiwa kumchagua raisi wao miongoni mwa wagombea 27 walioidhinishwa na tume ya uchaguzi na mshindi wa kinyang'anyiro hicho ndiye atakayefanikisha uundwaji wa serikali ya muungano wa kitaifa.

Taarifa toka nchini humo zinadokeza kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Taifa hilo Ibrahim Boubacar Keita anaongoza katika matokeo ya awali yaliyokwishahesabiwa katika baadhi ya vituo.

Aidha Waziri Modibe Sidibe ambaye naye ni Waziri Mkuu wa zamani na Soumaila Cisse ambaye ni Waziri wa zamani wa fedha wanaonyesha dalili za kupata uungwaji mkono katika kura hizo.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa na wizara ya mambo ya ndani siku ya jumanne.

Endapo hakutakuwa na mgombea aliyeibuka na kura nyingi zaidi basi duru la pili la uchaguzi huo litafanyika tarehe 11 ya mwezi Agosti na kuwashirisha wagombea waliopata zaidi ya asilimia 50.