ISRAELI-PALESTINA-MAREKANI

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yaanza jijini Washington

REUTERS

Wajumbe toka Israel na Palestina wameanza mazungumzo ya amani jumanne hii jijini Washington nchini Marekani kwa mara ya kwanza tangu jitihada hizo zilipokwama miaka mitatu iliyopita, Marekani imehimiza wawakilishi wa pande zote kufanya jitihada thabiti za kufikia makubaliano chanya.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amekaribisha ujumbe wa pande hizo mbili ambapo atahodhi mkutano huo, Martin Indyk ni Mjumbe wa Marekani kwenye mazungumzo hayo.

Tzipi Livni ni msuluhishi mkuu kutoka Israel ndani ya mazungumzo hayo na amesema kuwa nchi yake haipaswi kukata tamaa katika mchakato wa kupatikana amani kati ya mataifa hayo mawili.

Mazungumzo ya awali yalipangwa kufanyika jumatatu na jumanne jijini huku viongozi wa pande zote wakihimizwa kuwa tayari kufanya maamuzi magumu katika kuelekea kupatikana amani.

Rais Obama amepokea kwa mikono miwili hatua ya kuanza kwa mazungumzo kati ya Israel na Palestina na kusema kuwa Marekani iko tayari kuunga mkono pande hizo ili kufikia malengo yake.

Mazungumzo hayo yameanza siku moja baada ya Israel kuidhinisha uamuzi wa kuachiwa huru kwa wafungwa zaidi ya 100 wa Kipalestina.

Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita Waziri Mkuu Kerry amefanya ziara sita tofauti katika eneo la Mashariki ya Kati ili kuhimiza pande zote kukubali kurejea katika meza ya mazungumzo.