DRC-M23-UN

Umoja wa Mataifa watoa onyo kali Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

AFP PHOTO/PHIL MOORE

Umoja wa Mataifa umetoa muda wa saa 48 kwa makundi yote yanayomiliki silaha Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC hususani katika mji wa Goma kuzisalimisha mara moja, aidha umoja huo umetahadharisha kuwa unaweza kutumia nguvu dhidi ya kundi lolote litakalokaidi agizo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRCongo, MONUSCO imesema kundi linaloviziwa zaidi ni lile la waasi wa M23 huku operesheni hiyo ikilenga pia makundi mengine ya wapiganaji.

Brigedi maalumu ya Umoja wa Afrika AU inayowashirikisha wanajeshi toka Tanzania, Afrika Kusini na Malawi inatarajiwa kutumika kwa mara ya kwanza ili kulisaidia jeshi la DRCongo katika oparesheni hiyo.

Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 walianzisha mashambulizi dhidi ya jeshi la DRCongo katika mji wa Goma tarehe 14 ya mwezi huu.

Wanadiplomasia wameeleza kuwa mapigano hayo yamesababisha mamia ya raia kuuawa na wengine zaidi ya 5000 kuyahama makazi yao.

Wataalamu toka Umoja wa Mataifa UN pamoja na serikali ya DRCongo wamekuwa wakiishutumu Rwanda kuwafadhili wapiganaji wa M23 tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa vikali na serikali ya Kigali. Juma lililopita Washington pia iliionya Rwanda kuacha kuwaunga mkono wapiganaji hao.

Mashirika ya kiraia Mashariki mwa DRCongo yametoa wito kwa serikali ya Kinshasa na Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuidhibiti Rwanda na Uganda ambao wanadaiwa kuendelea kuwasaidia waasi wa M23 kwa kutuma majeshi yao Mashariki mwa DRCongo.