ZIMBABWE

Wananchi wa Zimbabwe wapiga kura katika uchaguzi mkuu

Reuters/路透社

Raia wa Zimbabwe wanapiga kura katika uchaguzi mkuu unaofanyika jumatano hii, mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgani Tsvangirai. Mugabe anawania tena nafasi hiyo aliyoishikilia katika kipindi cha miaka 33 ya utawala wake.

Matangazo ya kibiashara

Takribani watu milioni 6.4 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi huo kwenye vituo 9670 vilivyoandaliwa nchi nzima, aidha wapiga kura watatakiwa kuwachagua wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa.

Mshindi wa kiti hicho atatakiwa kupata asilimia 50 ya kura zote, idadi ambayo wagombea wote na vyama vyao wamejinadi kuwa lazima wataifikisha.

Mugabe ameahidi kukubali matokeo ikiwa atashindwa katika uchaguzi huo na amehakikisha kuwa Jeshi litaheshimu ushindi wa mgombea mwingine yeyote.

Mugabe mwenya umri wa miaka 89 anashiriki kinyang'anyiro hicho kwa mara ya saba, huku Taifa hilo likiendelea kukabiliwa na mfululizo wa migogoro ya kisiasa na kiuchumi.

Chama cha Movement for democratic Change MDC cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai kimedai kinao ushahidi juu ya mpango wa kukiukwa kwa sheria za uchaguzi, malalamiko hayo yamewasilishwa kwa waangalizi kutoka Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Africa SADC.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya nchi hiyo, Waandishi wa habari hawaruhusiwi kutangaza matokeo ya awali mpaka pale matokeo rasmi yatakapokamilika. Matokeo rasmi yanatarajiwa kuwa tayari ndani ya siku tano.

Matokeo hayo yatahitimisha serikali ya umoja kati ya chama Mugabe ZANU-PF na kile cha Tsvangirai cha MDC, serikali hiyo iliundwa ili kupata suluhu ya machafuko yaliyozuka mara baada ya uchaguzi ya mwaka 2008.