MISRI-MAREKANI

Wafuasi wa Morsi wakaidi amri ya kutoandamana wakati Marekani ikiitaka Misri kuheshimu uhuru wa kukusanyika

Wafuasi wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiandamana mjini Cairo
Wafuasi wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiandamana mjini Cairo REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Maelfu ya wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi wamekaidi onyo jipya lililotolewa na baraza la kijeshi na kuendelea kuandamana katika mji mkuu, Cairo.

Matangazo ya kibiashara

Chama cha Muslim brotherhood na wafuasi wamebainisha kuwa hawana uamuzi mwingine zaidi ya kutaka kiongozi wao arejeshwe madarakani.

Aidha Marekani imeitaka Misri kuheshimu uhuru wa watu kukusanyika , huku Bunge likipendekeza kusitisha misaada nchini Misri baada ya kuangushwa kwa Rais wa Taifa hilo, Mohamed Morsi.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani Marie Harf ametoa wito kwa Serikali ya mpito na Vikosi vya Usalama kuheshimu haki ya kuandamana kwa amani na kupiga kambi, hatua ambazo Serikali ya Misri imekuwa ikizuia kwa kile inachodai kuwa tishio kwa usalama wa Taifa.

Serikali ya Rais Barack Obama imekwepa kubatilisha mapinduzi dhidi ya Morsi, ambapo ingelazimu Marekani kusitisha misaada ya kiasi cha dola bilioni 1.5 kila mwaka.

Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani imesisitiza kuwa kutositisha misaada ni jambo muhimu kwa maslahi ya usalama wa Marekani na kwa ajili ya jitihada za kuishawishi Misri kuelekea kwenye Mchakato wa kidemokrasia