JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Francois Bozize: Nitarejea madarakani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

- Africanarguments.org

Rais aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya mwezi machi mwaka huu nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati, Francois Bozize amesema yupo tayari kurejea madarakani na kuiondoa serikali ya mpito inayoongozwa na kundi la waasi wa Seleka.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kuwa nje ya nchi yake kwa zaidi ya miezi minne, Bozize amesema atatumia njia za kidemokrasia kufanikisha lengo hilo na ikishindikana atalazimika kutumia nguvu.

Akiwa katika mahojiano na Radio France International RFI jijini Paris Ufaransa, Bozize ameituhumu nchi jirani ya Chad kwa kuwaunga mkono waasi wa Seleka waliofanikisha kuuangusha utawala wake.

Katika hatua nyingine, Bozize amesema ameanzisha chama chake ambacho anaamini kitamsaidia kufanikisha malengo hayo na ameiomba Ufaransa kusaidia Taifa lake ili suluhu ya kisiasa iweze kupatikana.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki-moon alilitaka Baraza la Usalama la UNSC kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa Seleka kutokana na kutajwa kuhusika na uvunjifu wa haki za binadamu nchini mwao.

Aidha Ban alihimiza uundwaji wa tume ya kutafuta ukweli itakayochunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea kushuhudiwa nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati.