MALI

Wananchi wa Mali waanza kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais

Reuters / Penney

Wananchi wa Mali hii leo wanashiriki zoezi la upigaji kura katika duru ya pili la uchaguzi wa Rais ambapo wagombea wawili walioongoza katika duru ya kwanza wanachuana kwa mara nyingine. Takribani vituo vya kupigia kura elfu ishirini na moja vimefunguliwa mapema leo asubuhi kwa ajili ya zoezi hilo katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa zamani wa Mali Ibrahim Boubacar Keita aliongoza kwa jumla ya asilimia 39.8 akifuatiwa na mpinzani wake Soumaila Cisse aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa fedha nchini humo ambaye alipata asilimia 19.7 ya kura zote.

Asilimia 49 pekee ya wapiga kura waliojiandikisha ndio waliojitokeza kupiga kura katika duru ya kwanza mwishoni mwa mwezi uliopita.

Keita amehimiza wananchi wa Taifa hilo kumchagua na anasema vipaumbele vyake ni kuwaunganisha wananchi wa Mali, kulijenga upya jeshi la nchi hiyo, kutengeneza nafasi za ajira na kuboresha elimu.

Keita mwenye umri wa miaka 63 na Cisse mwenye umri wa miaka 63 wamewahi kuwania pamoja Urais wa Mali mwaka 2002, mshindi wa uchaguzi huo alikuwa ni Rais aliyepinduliwa mwaka jana Amadou Toumani Toure, Cisse alishika nafasi ya pili na Keita nafasi ya tatu.

Umoja wa Mataifa UN umekuwa ukisisitiza umuhimu wa uchaguzi huo ili kusaidia kurejesha utawala wa kidemokrasia na kuanzishwa kwa majadiliano ya kitaifa yatakayosaidia kuweka makubaliano ya kitaifa.