Uingereza-Marekani

Muandishi wa habari aliekuwa akifanya kazi na Edward Snowden aghadhabishwa na hatuwa ya kushikiliwa kwa zaidi ya saa tisa nchini Uingereza

Glenn Greenwald akiwa pamoja na mshirika wake David Miranda
Glenn Greenwald akiwa pamoja na mshirika wake David Miranda REUTERS/Ricardo Moraes

Mamlaka ya nchini Uingereza ilimkamata na kumshikilia kwa saa tisa mshirika wa karibu wa mwaandishi wa Habari aliyekuwa akifanya kazi na Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la kijasusi la Marekani, Edward Snowden kutoa siri juu ya shughuli za kijasusi za Marekani. Hatuwa hii inakuja baada ya kumshuku kwamba bado anashikilia siri nyingine nyingi za shirika la kijasusi la Marekani CIA.

Matangazo ya kibiashara

David Miranda, Mshirika wa karibu wa Glenn Greenwald, Muandishi wa Habari wa kimarekani anayefanyia kazi Gazeti la nchini Uingereza, alikamatwa na kushikiliwa chini ya Sheria ya kupambana na Ugaidi siku ya jumapili alipokuwa uwanja wa ndege wa Heathrow akielekea mjini Rio de Janeiro akitokea Berlin.

Akiwa ameghadhabishwa na hatua hiyo, Greenwald amesema Mamlaka ya Uingereza haina uthibitisho wowote kuwa Miranda alihusika na vitendo vya kigaidi badala yake walimshikilia kwa saa kadhaa na kumuuliza maswali juu ya Ripoti ya Gazeti la Guardian juu ya Shughuli za Shirika la Kijasusi la Marekani, Ripoti iliyoighadhabisha Washington.

Greenwald amesema kuwa hatua hii inalenga kutoa ujumbe wa vitisho kwa Waandishi wa habari wanaoripoti juu ya Shirika la kijasusi la Marekani na Uingereza.

Miranda amezuiwa kupata Mwanasheria, huku maafisa usalama wakichukua vifaa vyake ikiwemo simu yake ya mkononi.