NIGERIA-BOKO HARAM

Marekani yataka ukweli kuhusu taarifa ya kuawa kwa kiongozi wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria

Abubakar Shekau, kiongozi wa Boko Haram nchini Nigeria
Abubakar Shekau, kiongozi wa Boko Haram nchini Nigeria

Utata juu ya kifo cha Kiongozi wa Kundi la Wanamgambo wa Kiislam la Boko Haram la nchini Nigeria Abubakar Muhammad Shekau umeifanya Serikali ya Marekani kuingilia kati na sasa inataka kufanya uchunguzi wa kina kupata ukweli wa taarifa hizo.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Marekani inajiandaa kupeleka wataalam wake nchini Nigeria kwa ajili ya kufanya uchunguzi kubaini ukweli wa taarifa zilizozagaa nchini humo ya kwamba Kiongozi wa Kundi la Boko Haram ameuawa licha ya kushindwa kuthibitishwa kwa taarifa zenyewe.

Msemaji Msaidizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Marie Harf amesema wamepata taarifa hizo lakini wangependa kupata ukweli juu ya maelezo yaliyotolewa na Jeshi ambalo limeshuhudia Viongozi wake wakishindwa kutoa maelezo zaidi.

Taarifa zilizotolewa mapema juma hili na Jeshi la Nigeria zilidai huenda Kiongozi wa Boko Haram Shekau aliuawa kwenye masgambulizi yaliyofanywa na Kikosi kazi kati ya tarehe ishirini na tano mwezi Julai hadi tarehe tatu mwezi Agosti.

Tangu kutolewa kwa taarifa hizo Jeshi limekuwa likishindwa kujitokeza hadharani na kuthibitisha kile walichokisema licha ya hapo awali Kundi la Boko Haram kutoa video inayomuonesha Shekau akiwa amejeruhiwa begani.