DRCONGO-MONUSCO

Watu wawili wauwawa kwa makombora mjini Goma Mashariki mwa DRC baada ya kikosi kipya cha Umoja wa Mataifa kuanza kuchukua hatua dhidi ya waasi

Kikosi Maalum Cha Umoja wa Mataifa UN kilichopelekwa nchini DRC kukabiliana na Makundi yanayomiliki silaha
Kikosi Maalum Cha Umoja wa Mataifa UN kilichopelekwa nchini DRC kukabiliana na Makundi yanayomiliki silaha un.org

Watu wawili wameuwawa kwa makombora huko Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC jana Jumamosi baada ya kikosi kipya cha umoja wa mataifa UN kuanza kutekeleza hatua za kijeshi kulisaidia jeshi la serikali na kuwazuia waasi kuingia katika eneo hilo lenye madini. 

Matangazo ya kibiashara

Walinda amani wa umoja wa mataifa UN walijeruhiwa kwa makombora ambayo yalianguka karibu na kituo chao, kikosi cha MONUSCO kimearifu na kudai kwamba wamekuwa wakilengwa na waasi.

Hata hivyo haijajulikana ni nani amehusika na kurusha kombora hilo ambalo limeuharibu mji wa Ndosho ulioko Magharibi jirani na Goma, na hivyo kuzua hasira kwa wakazi ambao walizuia njia ya magari, mashahidi wamesema.

Mjumbe wa umoja wa mataifa kwenye ukanda wa maziwa makuu Mary Robinson amelaani vurugu hizo akisema kwamba mashambulizi katika mji wa Goma na kwenye majeshi ya MONUSCO pamoja na madhara yake kwa raia hayakubaliki.