SYRIA

Msafara wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa washambuliwa Syria

Msafara wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa njiani kwenda karibu na mji wa Damascus nchini Syria kuanza kuchunguza ikiwa silaha za kemikali zilitumiwa kutekeleza shambulizi wiki iliyopita umeshambuliwa.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa hata hivyo haujasema ni nani aliyeshambulia msafara huo, ila imebainika kuwa gari la kwanza katika msafara huo lilivamiwa na kusababisha wachunguzi hao kurudi walikokuwa wametoka.

Uchunguzi huo ulitarajiwa kuanza siku ya Jumatatu siku moja baada ya serikali ya rais Bashar Al Assad kukubali kufanyika kwa uchunguzi huo baada ya waasi kuituhumu serikali  kutumia silaha za kemikali dhidi ya wafuasi wao.

Watalaam hao 20 wamekuwa Syria tangu tarehe 18 mwezi huu kuchunguza maeneo matatu yanayodhaniwa silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya wapinzani miezi kadhaa iliyopita.

Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.

Akihojiwa na gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia Assad amesisitiza kuwa Marekani haitafaulu na kamwe hawezi kuwa kibaraka cha mataifa ya Magharibi na ataendelea kupambana na makundi ya kigaidi yanayolenga kuiangusha nchi yake.

Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani , nchi yake itaivamia kijeshi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza William Hague naye amesema kuwa ikiwa silaha hizo zilitumiwa ni sharti hatua zichukuliwe lakini anahofia kuwa huenda ushahidi wa kufahamu ukweli umeshaharibiwa.

Serikali ya Assad imeendelea kusisitiza kuwa haiwezi na haijawahi kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani na itafanya hivyo ikiwa nchi yake itavamiwa na watu kutoka nje.

Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.

Suluhu ya mzozo wa Syria inasalia kuwa kitendawili baada ya juhudi za Kidiplomasia kugonga mwamba.