ISRAEL-PALESTINA

Mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel yaahirishwa

Mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israeli yaliyokuwa yamepangwa kufayika siku ya Jumatatu yaliahirishwa katika dakika za lala salama baada ya raia watatu wa Palestina kupigwa risasi na kuuawa katika Ukingo wa Magharibi.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, Marekani ambayo inafadhili mazungumzo hayo imekanusha kuahirishwa kwa mazungumgo hayo ya amani ambayo yalikuwa yameratibiwa kufanyika mjini Jericho.

Raia hao wa Palestina walipigwa risasi katika kambi ya wakimbizi wakati wakikabiliana na wanajeshi wa Israel mauaji ambayo Palestina inasema ni ukiukwaji wa haki za binadamu na yanaathiri mazungumzo hayo ya amani.

Palestina inasema haijui mazungumzo hayo yatarejelewa lini lakini Marekani kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje Marie Harf aliwaambia waandishi wa habari jijini Washington DC kuwa mazungumzo hayo bado yanaendelea.

Mazunguzo ya hivi karibuni ya moja kwa moja kati ya Palestina na Israel yalianza tarehe 29 mwezi uliopita baada ya kufanikiwa kwa juhudi za Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Israel ilikubali kuwaachilia huru wafungwa 104 wa Kipalestina ili kufanikisha kuanza kwa mazungumzo hayo ya amani yaliyokwama mwaka mmoja uliopita.

Palestina imekuwa ikiituhumu Israel kwa kutotaka mazungumzo hayo ya amani kwa kuendelea kujenga makaazi ya walowezi katika ardhi yao.