SYRIA-MAREKANI

Uingereza kuwasilisha azimio UN kuhusu Syria

Uingereza imesema itawasilisha azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya serikali ya Syria na kuwalinda raia dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu David Cameron amesema kuwa Baraza hilo la Usalama lina jukumu la kuhakikisha kuwa hatua madhubuti zinachukuliwa dhidi ya uongozi wa rais Bashar Al Assad anaosema umeendelea kuua raia wasiokuwa na hatia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon naye ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza hilo Marekani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China kuungana na kuzungumza kwa sauti moja ili kuiokoa Syria na kumaliza umwagaji damu.

Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo huo wa Syria Lakhdar Brahimi, amesema kuwa itakuwa sahihi kwa hatua za kijeshi kuchukuliwa dhidi ya Syria baada ya kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wachambuzi wa siasa na usalama wanaona kuwa haitakuwa rahisi kwa azimio lolote linalolenga kuishambulia Syria kupitishwa kutokana na Urusi na China ambazo ni washirika wa karibu wa serikali ya Damascus.

Wakati hayo yakijiri Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa hakuna shaka kuwa serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake.

Biden anakuwa kiongozi wa pili wa juu wa Marekani kutoa kauli hiyo na kusisitiza kuwa  ushahidi uko wazi na kila mtu ameona kuwa serikali ya rais Bashar Al Assad imewaua watu wake na ni lazima awajike.

Marekani inasema kuwa jeshi lake liko tayari kuongoza mashambulizi  dhidi ya Damascus na uamuzi wa rais Barrack Obama unasubiriwa ili hatua ichukuliwe.

Siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya nje wa Syria Walid Moualem aliitaka dunia kutoa ushahidi kuwa serikali yake ilitumia silaha za kemikali wiki iliyopita dhidi ya wapinzani na kusababisha vifo vya mamia ya watu mjini Damascus.

Syria inasema Marekani na washirika wake wanaidanganya dunia kwa sababu wanatafuta njia ya kuingia nchini humo, na kuongeza kuwa wako tayari kujilinda ikiwa watashambuliwa.

Nchi za Urusi na Iran nazo zimesema kuwa hatua yeyote ya kijeshi dhidi ya Syria bila ya kupitia katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haikubaliki na ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon ameitisha kikao cha dharura cha wabunge siku ya Alhamisi kujadili mustakabali wa Syria kipindi hiki dalili zikionesha kuwa mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yanajiandaa kuivamia Syria.

Duru kutoka Washington DC zinasema kuwa jeshi la Marekani lipo tayari kuongoza mashambulizi hayo, huku uongozi wa upinzani nchini Syria ukisema kuwa umeambiwa kuwa watarajie mashambulizi  dhidi ya serikali ya rais Assad katika siku kadhaa zijazo.

Marekani na washirika wake kama Ufaransa na Uingereza wanasema wakati umefika kwa Syria kuvamiwa kijeshi pendekezo ambalo washirika wa karibu wa rais Assad China na Urusi wanapinga.

Leo ni siku ya tatu ya uchunguzi unaofanywa na watalaam wa Umoja wa Mataifa kubaini ikiwa kweli silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia wasiokuwa na wakati.

Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.

Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani,nchi yake itaivamia kijeshi.

Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.