MAREKANI-SYRIA

Ban Ki Moon kupokea ripoti kuhusu silaha za kemikali nchini Syria siku ya Jumamosi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema siku ya Jumamosi atapokea ripoti kutoka kwa wachunguzi wanaothathmini  ikiwa silaha za kemikali zilitumiwa karibu na mji wa Damascus nchini Syria wiki iliyopita katika shambulizi lililosababisha mamia ya watu kuuawa.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatano,  Moon alisema kuwa itawachukua wachunguzi  hao siku nne kumaliza kazi yao na uamuzi wowote kuhusu Syria unaweza kuchukuliwa baada ya uchunguzi huo kumalizika na ripoti kutolewa.

Ripoti hiyo inasubiriwa  huku rais wa Marekani Barrack Obama akisema kuwa serikali yake imeshafikia uamuzi kuwa serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali kuwavamia raia wasiokuwa na hatia karibu na mji wa Damascus wiki iliyopita.

Obama amesema kuwa matumizi ya silaha hizo zimeathiri maslahi ya taifa la Marekani na huenda yakawa na matokeo mabaya kuhusu mgogoro huo wa Syria.

Hata hivyo, rais Obama amesema kuwa hajaamua ikiwa jeshi lake litaivamia Syria kijeshi siku moja baada ya azimio la Uingereza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka raia wa Syria kulindwa kushindwa.

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Syria ilipinga azimio hilo na kusema kuwa itaunga mkono azimio litakalosaidia kumaliza mzozo wa Syria Kidiplomasia.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anatarajiwa kulihotubia bunge siku ya Alhamisi kuhusu mzozo wa Syria na kuwaomba kuunga mkono juhudi za serikali kuungana na  mataifa mengine kuchukua hatua dhidi ya Damascus.

Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo huo wa Syria Lakhdar Brahimi, naye amesema itakuwa sahihi kwa hatua za kijeshi kuchukuliwa dhidi ya Syria baada ya kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wachambuzi wa siasa na usalama wanaona kuwa haitakuwa rahisi kwa azimio lolote linalolenga kuishambulia Syria kupitishwa kutokana na Urusi na China ambazo ni washirika wa karibu wa serikali ya Damascus.

Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.

Mwaka uliopita, rais Obama alionya kuwa ikiwa serikali ya Syria itatumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani,nchi yake itaivamia kijeshi.

Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.