MAREKANI-SYRIA

Ufaransa yasema iko tayari kuisaida Marekani kuishambulia Syria

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa anaunga mkono hatua ya Marekani kuongoza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Syria baada ya kutokea kwa shambulizi la silaha za kemikali nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Matangazo ya kibiashara

Paris inasema kinachotokea nchini Syria hakikubaliki kamwe na ni  lazima serikali ya Assad ichukuliwe hatua ili kukomesha machafuko yanayoendelea nchini humo.

Rais Hollande amesema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Marekani katika oparesheni hiyo suala ambalo wachambuzi wa siasa wanasema imeipa nguvu serikali ya Marekani.

Kauli ya Ufaransa inakuja huku Marekani ikisema itachukua hatua dhidi ya nchi ya Syria kwa kuzingatia maslahi yake baada ya wabunge wa Uingereza kupinga mswada wa serikali kulishirikisha jeshi lake katika mzozo wa Syria.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema kuwa baada ya uamuzi wa bunge la Uingereza, Marekani itaendelea kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa mataifa mengine ili kuichukulia hatua serikali ya Syria kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake.

Marekani imeituhumu serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali kuwavamia raia wake wasiokuwa na hatia, na kuvunja sheria za kimataifa kuhusu silaha hizo tuhma ambazo serikali ya rais Bashar Al Assad imeendelea kukanusha.

Hatua ya wabunge wa Uingereza kupinga mswada uliokuwa umewasilishwa na Waziri Mkuu David Cameron siku ya Alhamisi inaaminisha kuwa Uingereza haitahusika kijeshi katika uvamizi wa Syrai kijeshi utakaoongozwa na Marekani.

Wabunge wa Uingereza waliopinga mswada huo walisema kuwa walihofia matokeo ya baada ya uvamizi huo na kuendelea kuuawa kwa wananchi wa Syria na mzozo huo kusambaa katika mataifa jirani kama ilivyokuwa nchini Iraq na Libya.

Wachambuzi wa siasa za Kimataifa wanasema kuwa hatua ya wabunge wa Uingereza kukataa jeshi lao kuhusika na mzozo wa Syria ni pigo kwa Marekani na sasa itabidi itafute uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Ufaransa ,Ujerumani na mataifa mengine.

Serikali ya Ufaransa imeonekana kuunga mkono matumizi ya jeshi nchini Syria baada ya rais Francois Hollande kunukuliwa akisema kuwa kinachoendelea nchini humo hakikubaliki na wakati wa kutumia jeshi umefika.

Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe na yuko tayari kujilinda.

Siku ya Alhamisi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alisema kuwa atapokea ripoti kutoka kwa wachunguzi wanaothathmini  ikiwa silaha za kemikali zilitumiwa karibu na mji wa Damascus siku ya Jumamosi.

Moon anasema hatua yeyote dhidi ya Syria ni sharti ichukuliwe baada ya kukamilika kwa ripoti ya wachunguzi hao.

Machafuko nchini Syria yamesabisha zaidi ya watu Laki Moja kupoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwli iliyopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, na Mamilioni kusalia kuwa wakimbizi wakiwemo watoto.