SYRIA-UN

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa waondoka Damascus baada ya kukamilisha uchunguzi wa silaha za kemikali

Wataalamu wa maswala ya kemikali wa Umoja wa Mataifa UN waliokuwa nchini Syria wameondoka asubuhi ya leo jumamosi baada ya kukamilisha uchunguzi wao wa kubaini iwapo silaha za kemikali zilitumika katika mapigano. Wataalamu hao wamekamilisha uchunguzi wao wa siku nne katika eneo linalolalamikiwa kuwa silaha za kemikali zilitumika dhidi ya raia pembezoni mwa mji mkuu Damascus tarehe 21 ya mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Jumla ya Wachunguzi hao 13 wanaoongozwa na Ake Sellstrom wameondoka kupitia Beirut nchini Lebanon ambapo walionekana wamebeba mizigo yao katika magari saba ya UN.

Kuondoka kwa wataalamu hao kunatajwa kama hatua mojawapo ya kukaribia kupata ukweli unaotafutwa sambamba na kujua mustakabali wa uamuzi wa uvamizi wa kijeshi unaopigiwa upatu na Marekani.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa UN wanasema huenda itachukua majuma mawili kupata majibu ya utafiti huo na kukabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon.

Msemaji wa UN, Martin Nesirky amesema wataalamu hao watarejea tana kuchunguza maeneo mengine yanayodaiwa silaha za kemikali zilitumika katika mapigano ya kuupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad yaliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Wakati huo huo Marekani na Uingereza zimesisitiza kuwa uhusiano wao haupo hatarini kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu kutokana na bunge la Uingereza kupinga pendekezo la kuvamia kijeshi nchi ya Syria inayoshutumiwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake.

Katika mazungumzo ya simu baina ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa Marekani Barack Obama, Obama amemthibitishia Cameron kuheshimu maamuzi wa bunge, Ofisi ya Cameron imethibitisha.

Viongozi hao wamekubaliana kuendeleza ushirika wao katika maswala ya kimataifa na kwa pamoja kuendeleza dhamira yao ya kusaka suluhu ya kisiasa juu ya mgogoro wa Syria.

Marekani imeendelea kutafuta uungwaji mkono katika suala hili, tayari Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameunga mkono hatua hiyo na kusema ni lazima hatua ichukuliwe ili kukomesha machafuko hayo.