MAREKANI-SYRIA

Rais wa Marekani Barrack Obama kuomba idhini ya bunge kabla ya kuivamia kijeshi nchi ya Syria

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajia kuomba idhini ya bunge la nchi hiyo ili aweze kufanikisha mkakati wa kuivamia kijeshi nchi ya Syria inayotuhumiwa kwa matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia wake. Kwa mujibu wa katiba ya nchi yake, Rais Obama anayo haki ya kuliagiza jeshi lake kuvamia Syria bila kuomba idhini ya bunge lakini jeshi hilo halitatakiwa kukaa vitani kwa zaidi ya siku 60 ikiwa bunge halikuidhinisha uvamizi.

REUTERS/Jonathan Ernst
Matangazo ya kibiashara

 

Bunge la Congress linatarajiwa kupigia kura pendekezo hilo kabla ya tarehe 9 mwezi huu na Rais Obama sasa anasema kuna umuhimu wa kuwa na majadiliano kabla ya hatua za kijeshi kuchukuliwa.

Katika taarifa fupi iliyotolewa kwa waandishi wa habari mwishoni mwa juma hili kwenye ikulu ya White House, Obama amesema jeshi la Marekani lipo tayari kwa uvamizi ili kumuadabisha Bashar al-Assad kutokana na majeshi yake kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria.

Marekani inasema ina uthibitisho kuwa majeshi ya serikali ya Damascus yalitumia silaha hizo katika shambulizi la Agosti 21 pembezoni mwa mji wa Damascus ambapo watu zaidi ya 1,000 walidaiwa kufa.

Serikali ya Syria imekuwa ikikanusha tuhuma zinazoelekezwa kwake na kuwataja waasi kuwa ndio waliotumia silaha za kemikali.

Naye mshirika wa karibu wa serikali ya Damascus, Rais wa Urusi Vladmir Putin ameisisitiza Marekani kuweka hadharani ushahidi wake unaoonyesha kuwa silaha za kemikali zilitumiwa na majeshi ya Assad.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande anaunga mkono pendekezo la uvamizi wa kijeshi na bunge la nchi hiyo linatarajia kupigia kura iwapo wanataka kujiunga na Marekani kwenye oparesheni hiyo.

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN waliokuwa nchini humo kuchunguza iwapo silaha za kemikali zilitumika wameondoka mjini Damascus siku ya jumamosi wakiwa na sampuli walizochukua toka eneo la tukio tayari kwa kuzipeleka maabara ili kupata majibu sahihi.