MAREKANI-SYRIA

Rais Barack Obama aanza harakati za kusaka uungwaji wa mkono ili aishambulie Syria

REUTERS/Mike Theiler

Rais wa Marekani Barack Obama ameanzisha harakati za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wabunge kabla ya kuidhinisha mpango wa kuivamia kijeshi nchi ya Syria kwa madai kuwa majeshi ya serikali ya Syria yalitumia sihaha za kemikali. 

Matangazo ya kibiashara

Rais Obama anayo haki kisheria kuidhinisha uvamizi huo bila idhini ya bunge lakini amesema ni muhimu majadiliano kufanyika kwanza kabla ya kusonga mbele.

Uamuzi huo umekuja wakati Washington ikizidi kusisitiza kuwa inao uthibitisho kuwa serikali ya Damascus ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika shambulio la Agosti 21.

John Kerry ni Waziri wa mambo ya nje nchi hiyo na amesema wamethibitisha kuwa sumu aina ya sarin ilitumika dhidi ya raia.

Wakati huo huo, Mawaziri wa nchi za nje wa jumuiya ya kiarabu wanaokutana mjini Cairo wametoa wito kwa Marekani na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha hatua wanazochukua hazivunji Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Serikali ya Syria imeendelea kukanusha kuwa imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake huku upande wa upinzani ukiendelea kuilaumu serikali ya Bashar Al Assad kwa kutumia silaha kemikali.

Marekani na washirika wake wanajipanga kuishambulia Syria huku Umoja wa Mataifa ukisubiri ripoti ya timu yake ya uchunguzi wa matumizi ya silaha za kemikali.