DRCONGO-MONUSCO-M23

Risasi zaendelea kurindima Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Milio ya risasi imeendelea kusikika Mashariki mwa Jamuhiri ya Kidemokrasia ya Kongo karibu na mji wa Goma baada ya utulivu wa muda mfupi kufuatia makabiliano baina ya waasi wa M23 na majeshi ya serikali.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Hayo yanajiri wakati jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia, FARDC likisaidiwa na vikosi vya MONUSCO lilipofaulu kuwasambaratisha waasi wa kundi la M23 na kuwaondoa katika ngome muhimu ya minara mitatu waliokuwa wakidhibiti.

Hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda katika mpaka baina ya DRC na Rwanda baada ya kushuhudiwa vifaru vya kijeshi na wanajeshi wa Rwanda wakielekea katika mpaka wa Rwanda na DRCongo.

Wasiwasi huo umeendelea kutanda baada ya Rwanda kulituhumu jeshi la FARDC kuvurumisha kombora katika ardhi ya Rwanda na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja.

Katika hatuwa nyingine, polisi jijini Kinshasa imeusambaratisha mkutano wa upinzani uliokuwa umeandaliwa jana katika mji huo huku wapinzani kadhaa wakitiwa nguvuni.

Watu hao walitiwa nguvuni baada ya kuitisha mkutano wa hadhara kuwafahamisha wananchi kuhusu mpango wa marekebisho wa katiba kipengele nambari 220 ili kumruhusu rais Kabila kujichagulisha tena kuwa rais baada ya uchaguzi wa 2011 uliopingwa vikali na upinzani.