SYRIA-MAREKANI

Maseneta nchini Marekani wagawanyika kuhusu kuishambulia kijeshi Syria

Baadhi ya Maseneta nchini Marekani wamesisitiza kuwa ni lazima Washington ianzishe operesheni ya kijeshi dhidi ya Rais Bashar al-Assad ili kulinda heshima ya nchi hiyo na kukomesha ukiukwaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa Syria.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo wapo maseneta wengine wanapinga hatua hiyo na kusema wanaona hatua hiyo huenda ikaigharimu serikali ya Rais Barack Obama ambaye ameonyesha nia ya kuishambulia Syria kwa madai kuwa majeshi ya serikali yametumia silaha za kemikali dhidi ya raia.

Seneta John MacCain na Seneta Lindsley Gharam wa chama cha Republican wanaounga mkono pendekezo hilo, huku John Maccain akisema kutakuwa na matokeo mabaya endapo bunge litapinga pendekezo hilo.

Rais wa Marekani Barack Obama ameendelea kutafuta uungwaji mkono toka kwa bunge la nchi hiyo kabla ya kuivamia kijeshi nchi ya Syria wakati huu ambapo kumeshuhudiwa mgawanyiko kutokana na wengine kuonekana wakipinga pendekezo hilo.

Vikosi vya kujihami vya nchi za magharibi NATO vinasema vinaamini utawala wa Assad ulitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake lakini lazima wanachama 28 wa umoja huo wakiongozwa na Marekani wakubaliane ni hatua zipi zichukuliwe.

Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kuwa ikiwa watalazimika kufanya oparesheni ya kijeshi huko Syria ni lazima iwe ya muda mfupi na uhakika.