DRC-M23-UN

Umoja wa Mataifa wawataka waasi wa M23 wasalimishe silaha kumaliza machafuko DRC

REUTERS/James Akena

Umoja wa Mataifa, UN umewataka waasi wa kundi la M23 kuweka silaha chini ili kumaliza mapambano yanayofanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuleta athari mbaya kwa wananchi.

Matangazo ya kibiashara

Umoja huo umesema kumalizwa mapambano kati ya majeshi ya umoja huo na waasi wa M23 kutasaidia kupatikana kwa njia za kuleta suluhu baina ya pande hizo mbili.

Wito huo umetolewa na mjumbe maalum wa kanda ya Maziwa Makuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Mary Robinson ametoa wito huo wakati wa ziara yake mashariki mwa DRC eneo ambalo linakabiliwa na vita.

Hatua hiyo imekuja huku majeshi serikali ya Kongo yakishirikiana na majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiwa yamefanikiwa kuidhibiti ngome muhimu ya waasi wa M23.

Bi Robinson akiwa mjini Goma baada ya kuzungumza na viongozi wa serikali za mitaa na wakazi wa mji huo amesema kuwa waasi wa M23 lazima wakomesheshe mapambano na kusalimisha silaha kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bi. Robinson aliwasli nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku majeshi ya DRC yakijipanga kuikomboa ngome ya Kibumba inayoshikiliwa na waasi wa M23 iliyoko kilomita 30 kaskazini mwa Mji wa Goma.

Ijumaa iliyopita wapiganaji wa M23 walirudi nyuma kutoka katika maeneo waliyokua wakiyashikilia kuzunguka Mji wa Goma ambao waliwahi kuuteka kwa siku 12 mwezi Novemba mwaka jana kabla ya kuondoka kutokana na shinikizo la kimataifa.

Waasi hao walisema waliamua kusitisha mapigano siku ya Ijumaa ili kuweka mazingira ya kutafuta suluhu kwa njia za mazungumzo ya kisiasa inagawaje wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hizo ni dalili za kudhoofishwa kwa M23.