SYRIA-UN

Ban Ki-moon: Majibu ya jopo la wachunguzi yatathibitisha iwapo Syria ilitumia silaha za kemikali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki-moon amesema majibu ya ripoti juu ya matumizi ya silaha za kemikali yanayotarajiwa kutolewa juma lijalo yatathibitisha juu ya sintofahamu hiyo na kutoa mwelekeo wa mgogoro wa Syria uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili. Tayari kiongozi wa jopo la wataalamu wa uchunguzi huo, Ake Sellstrom amethibitisha kuwa ripoti hiyo ipo tayari na hivi karibuni wataiwasilisha kwa Katibu Mkuu wa UN.

REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo Ban ameeleza wasiwasi wake iwapo Syria itaonyesha ushirikiano wa kutosha katika swala la utekelezaji wa makubaliano ya kudhibiti matumizi ya silaha za sumu.

Aidha amemtuhumu waziwazi Rais Bashar al-Assad kuwa ametenda uhalifu dhidi ya watu wake na kusema kiongozi huyo atakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu hapo baadaye.
 

Msemaji wa Washington Marie Harf amesema anaamini ripoti hiyo haitakuwa na mtazamo tofauti na kile walichokisema hapo kabla kuwa majeshi ya Rais Assad ndiyo yaliyotumia silaha za kemikali katika shambulizi ya Agosti 21 pembezoni mwa mji wa Damascus.

Wakati huo huo Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi wanaendelea na mazungumzo juu ya mgogoro huo kwa siku huku wakitarajia kukutana tena ndani ya majuma mawili yajayo kupanga tarehe ya kuanza kwa mazungumzo ya pili kuhusu amani ya Syria mjini Geneva Uswiss.