TANZANIA

Padre wa Kanisa Katoliki visiwani Zanzibar ashambuliwa kwa kumwagiwa tindikali

Padre Anselmo Mwang'amba wa kanisa katoliki visiwani Zanzibar nchini Tanzania amemwagiwa tindikali na watu wasiofahamika akiwa katika eneo la Ngome Kongwe siku ya ijumaa. Kwa mujibu wa mashuhuda ni kuwa Padre huyo wa Parokia ya Machui alitokea kwenye internet cafe moja mjini hapo na dakika chache alirejea huku akipiga yowe kwa lengo la kuomba msaada.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Rukia Abbasi ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa cafe hiyo amesema walimpatia Padre huyo huduma ya kwanza kwa kumwagia maji na kisha kumkimbiza hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Madaktari wamesema wanaendelea kumtibu majeraha aliyopata maeneo ya usoni, kifuani na mikononi na endapo hakutakuwa na mabadiliko chanya basi watamsafirisha kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International, Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi visiwani humo Inspekta Mohammed Mhina amesema wanaendelea kuchunguza ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo na kuwaomba wananchi kushirikiana nao katika kuwasaka wahalifu hao.

Hili sio shambulio la kwanza kwa viongozi wa dini visiwani humo, mwezi Februari mwaka huu Padre Evarist Mushi alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiofahamika, wakati mwezi desemba mwaka jana Padri Ambrose Mkenda alinusurika kifo baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati akitoka kanisani kuhudhuria misa.

Aidha kiongozi wa dini ya kiislamu, Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar Shekh Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali mwezi Novemba mwaka jana na Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja Mohammed Omar Said alimwagiwa tindikali mwezi Mei mwaka huu.

Tukio la karibuni ni lile la wasichana wawili raia wa Uingereza waliokuwa wafanyakazi wa kujitolea visiwani humo kuvamiwa na kumwagiwa tindikali, mpaka hivi sasa watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajatiwa nguvuni licha ya kutangazwa donge nono la euro 4500 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwao.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikilaani vitendo hivyo ambavyo vinatia doa Taifa hilo la Mashariki mwa Afrika.