Marekani-Iran

Marekani yasema kuwa na matumaini kuiona Iran inarejea kwenye meza ya mazungumzo juu ya mpango wake wa Nyuklia

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack Obama REUTERS/Jason Reed

Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa atadhihirisha ukweli juu ya dalili kuwa Rais wa Iran Hassani Rohani yu tayari kufanya mazungumzo juu ya mpango wake tata wa Nyuklia na nchi za magharibi, mpango ambao unapingwa na mataifa yenye nguvu duniani.

Matangazo ya kibiashara

Obama amesema kuwa kuna fursa ya kuwepo kwa mazungumzo ya kidiplomasia na Iran na kuwa Iran itatumia fursa hiyo vyema kuwa kuwa Rais mpya wa nchi hiyo ana nia ya kufanya mazungumzo juu ya suala hilo, hali ambayo haikujionesha hapo mwanzoni.

Matumaini yaliyopo hivi sasa ni kuwa Mazungumzo kuhusu Nuklia kati ya Iran na Mataifa yenye nguvu duniani yanatarajiwa kuanza hivi karibuni hii ni kutokana na kauli ya Kiongozi wa juu wa kidini nchini Iran, Ayatollah Khamenei.

Mapema Jumanne, kiongozi mkuu, wa kidini nchini humo Ali Khamenei, ametoa wito kwa kulegeza msimamo katika majadiliano ya kidiplomasia. Iran na mataifa yenye nguvu yamepanga kuanzisha upya mazungumzo juu ya mpango wa Nyuklia wa Iran wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wakati ambapo kwenye ratiba ya rais Obama kwa sasa hakuna mpango wa kukutana na rais Rohani.

Washingtona na Washirika wake wanadai kuwa Mradi wa Nyuklia wa Iran unalenga kutengeneza silaha zilizopigwa marufuku kimataifa, taarifa ambayo imekuwa ikikanushwa na Iran. Hata hivyo Marekani haijatamka lolote kuhusu kuchukua hatua za kijeshi ikiwa mazungumzo ya kidiplomasia yatagonga ukuta.