DRC-M23-UN

Maadhimisho ya amani duniani, DRCongo yahimizwa kuchangia Juhudi za kuleta amani

Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa mataifa nchini DRC Monusco katika Jiji la Goma,
Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa mataifa nchini DRC Monusco katika Jiji la Goma, REUTERS/Thomas Mukoya

Dunia inaadhimisha leo Jumamosi siku ya Amani ambapo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wananchi wamejiandaa kushiriki Maandamano yatakayofuatiwa na hafla kubwa ya kuhimiza amani katika eneo hilo lililo kumbwa na mapigano ya mara kwa mara, na ambayo yamekuwa yakiyahusisha makundi ya waasi.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe hizo zenye lengo la kuwahimiza wananchi juu ya suala nzima la amani zimefanyika jijini Goma, katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini ambapo zimeandaliwa na tume ya umoja wa mataifa nchini Congo,ifahamikayo kama Monusco na katika Ushirikiano na mashirika mengine ya kimataifa.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na shirika la Search for common ground,kitengo cha mashariki mwa DRC, ni kuwa shughuli mbalimbali zikiwemo michezo, mashindano ya riadha zimepangwa kufanyika katika Siku hii inayoadhimishwa chini ya kauli-mbiu inayosema :Elimu na Amani, nitafanya nini.?

Viongozi wa serikali ya Jimbo la Kivu ya Kaskazini wameomba umoja wa mataifa na jumuia nzima ya kimataifa kuharakisha juhudi za kuimarisha amani katika kukomesha mapigano yanayokithiri sana katika eneo hilo la mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika maeneo mengine ya kaskazini mwa taifa hilo, raia waliokimbia mapigano mwishoni mwa mwezi wa Julai katika mji wa Kamango jimboni Kivu ya kaskazini kwenye mpaka baina ya Congo na nchi jirani ya Uganda wameomba serikali ya kinshasa na Umoja wa Mataifa kuhakikisha waasi wa Allied Democratic Forces, ADF-Nalu wanatokomezwa kufwatia vitendo vya utekaji nyara, mauaji na uporaji ,kama wanavyoendelea kufanya waasi hao kutoka Uganda.