KENYA

Idadi ya watu waliouawa Kenya yafikia 59 na majeruhi 175

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya Joseph Ole Lenku amesema idadi rasmi ya watu waliopoteza maisha imefikia 59 wakati majeruhi 175 wakitawanywa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi kupatiwa msaada wa kiafya.Aidha Ole Lenku ameeleza kuwa wanausalama bado wanazingira jengo la Westgate kuhakikisha watu waliotekwa na wapiganaji wa Alshabab wanaokolewa salama na watuhumiwa hao wanatiwa nguvuni.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa pole kwa jamaa waliopoteza ngudu zao katika tukio hilo na kuwataka raia wa Kenya kushikamana na kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wanausalama kukabiliana na tatizo hilo.

Wanamgambo hao wa kundi la kigaidi la Al Shabab wamesema walitekeleza shambulizi hilo kwa sababu serikali ya Kenya imekataa kuyaondoa majeshi yake nchini Somalia.

Tayari watu wengine wanne wametajwa na vyombo vya habari nchini humo kuokolewa kutoka ndani ya jengo hilo la biashara ambapo walishuhudia kuwa waliwaona watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakianza kumshambulia mtu yeyote waliyekutana naye ndani ya jengo hilo jumamosi mchana.

Inadaiwa kuwa washambulizi hao walikuwa wanamuuliza waliyekutana naye maswali ya Kislamu na yeyote aliyeshindwa kutoa jibu au kuthibitisha kuwa ni Mwislamu alipigwa risasi.

Rais Kenyatta ametaja shambulizi hilo la kigaidi kuwa ni kitendo ambacho hakikubaliki kamwe na waliohusika watakumbana na mkono wa sheria.

Aidha, Kenyatta amesisitiza kuwa wakenya hawatagawanyika kutokana na shambulizi hilo na jeshi lake litaendelea kukabiliana na magaidi nje na ndani ya taifa hilo.

Makundi mbalimbali nchini humo yamejitokeza kulaani shambulio hilo na kutoa pole kwa wahanga,akiwemo waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati mapambano hayo yanayoendelea nchini humo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ungereza William Hague amesema kuwa serikali yake inashirikiana na Kenya kuhakikisha kuwa inakabiliana na suala la ugaidi na wanamgambo hao wanapatikana.

Miongoni mwa raia wa kigeni waliopoteza maisha yao katika shambulizi hilo ni pamoja na raia wawili wa Ufaransa na Canada.

Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kuikumba Kenya tangu shambulizi la bomu lililotokea mwaka 1998 lilotekelezwa na Al-Qeada.