URUSI-EU-SYRIA

Urusi iko tayari kutuma ujumbe wake kusimamia uchunguzi na uteketezwaji wa silaha za kemikali nchini Syria

Serikali ya Urusi, imesema iko tayari kupeleka wanajeshi wake nchini Syria kusimamia zoezi la uchunguzi na uteketezwaji wa silaha za kemikali nchini Syria wakati huu kukitekelezwa shambulio la roketi nje ya ofisi za ubalozi wa Urusi mjini Damascus.

Waziri wa mambo ya Ulinzi wa Ufaransa Laurent Fabius, akiwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi  Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya Ulinzi wa Ufaransa Laurent Fabius, akiwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov REUTERS/Maxim Shemetov
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Urusi inatolewa wakati huu ambapo waasi nchini syria wametekeleza shambulio la roketi kulenga ofisi ya ubalozi wa urusi mjini damascus na kujeruhi watu watatu, shambulio ambalo Urusi imelaani.

Katika hatua nyingine nchi hiyo imesema iko tayari chini ya makubaliano yake na Marekani, kupeleka kikosi cha wanajeshi nchini Syria kushirikiana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa katika kubaini maeneo zinakohifadhiwa silaha za kemikali na kuziteketeza.

Lakini katika kile kinachoonekana huenda makubaliano kati ya Urusi na Marekani yakafutiliwa mbali, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, sergei Lavrov ameituhumu Marekani kwa kuendeleza juhudi za kuwashawishi wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kutumia nguvu kuivamia kijeshi nchi ya Syria.

Waziri Lavrov amesema anashangazwa na kitendo ambacho kinaendelea kufanywa na Marekani na washirika wake kwenye baraza la Umoja wa mataifa kuendelea kusambaza propaganda mbaya kuhusu utawala wa Syria kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono kuishambulia Syria.

Urusi imeendelea kusisitiza licha ya makubaliano yake na Marekani haiungi mkono matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya utawala wa Syria.