SYRIA-MAREKANI-URUSI-ISRAEL-UMOJA WA MATAIFA

Makubaliano ya mawaziri wa mambo ya kigeni hayajafua dafu,Mzozo kati ya Marekani na Urusi waendelea kufukuta

Waziri wa mambo ya kigeni Marekani John Kerry akiteta na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya kigeni Marekani John Kerry akiteta na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov rfi

Mzozo unaofukuta kati ya serikali ya Marekani na Urusi kuhusu namna ya kutatua mgogoro wa Syria pamoja na kuteketeza silaha zake za kemikali umeendelea kufukuta na huenda ikawa ajenda kubwa ya mkutano huu wa 68 wa umoja wa mataifa unaoanza hii leo jijini New York, Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Fukuto la mvutano kati ya nchi hizi mbili limeendelea kuongezeka hata kabla ya kuanza kwa mkutano wa baraza la Umoja wa mataifa, mvutano unaoibuka ikiwa zimepita siku chache toka mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Marekani wasaini makubalino ya hatua za kuchukua dhidi ya utawala wa Syria.

Mataifa ya magharibi yanadai kuwa msimamo wa Urusi kuendelea kupinga azimio lolote la Umoja wa mataifa kuhusu kuchukua hatua zaidi kwa utawala wa Syria, kunampa kiburi rais Bashar al-Assad ambaye wanadai wanajeshi wake wanaua raia wasio na hatia.

Juma hili, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ameishutumu nchi ya Marekani kwa kuendelea propaganda chafu dhidi ya utawala wa Assad kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono kutumia nguvu kuuangusha utawala wa Syria licha ya makubaliano waliyofikia.

Marekani na washirika wake wameendelea kusisitiza kuwa utawala wa rais Assad ndio uliotumia silaha za kemikali, tuhuma ambazo Urusi inapinga na kutaka kuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo kabla ya kukubaliana na azimio la Umoja wa mataifa kutumia nguvu dhidi ya Syria.