MAREKANI-IRAN-URUSI

Marekani kufanya mazungumzo na Iran juu ya nyuklia

Raisi wa Iran Hassan Rowhan anatarajia kukutana na raisi wa Marekani  Barack Obama
Raisi wa Iran Hassan Rowhan anatarajia kukutana na raisi wa Marekani Barack Obama Reuters/President.ir/Handout via Reuters

Katika kile kinachoonekana kuwa huenda diplomasia ikafanikiwa, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na Iran watakutana mjini New York Marekani wakati wa mkutano wa 68 wa Umoja wa mataifa unaonza hii leo kuzungumzia suala la Iran na mpango wake wa Nyuklia.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran, Mohammad Javaz Zarif watakutana na wenzao wa China, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Urusi kuzungumzia mzozo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi ya Iran.

Taarifa zinasema kuwa huenda rais wa Iran, Hassan Rowhan akakutana kwa mazungumzo ya faragha na rais wa Marekani Barack Obama wakati wa mkutano wa Umoja wa mataifa kuzungumzia suala hilo.
 

Kwa mara ya mwisho mazungumzo ya mpango wa Nyuklia yalifanyikia Kazakhstan mwezi April ingawa makubaliano yamekuwa yakigonga mwamba kwa muda wa miaka 8 sasa.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani unaozingatia haki za msingi za kimataifa na kupinga mpango wa baraza la usalama la umoja wa mataifa UN unaoitaka Iran kuacha urutubishaji wa madini ya uranium.

Tangu uchaguzi wa rais mpya, Hassan Rouhani, mwezi Juni, Tehran ilionyesha inaweza kuwa tayari kufanya makubaliano juu ya suala la nyuklia.