SOMALIA-KENYA

Raisi wa Somalia asema Alshabab walishirikiana na Al Qaeda kushambulia Westgate Nairobi

Wakati jeshi la Kenya likiarifiwa kudhibiti eneo zima la jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi,Rais wa Somalia, Hassan sheikh Mohamud amesema kuwa wanamgambo wa Al-Shabab waliotekeleza shambulio kwenye eneo hilo hawakufanya kazi peke yao bali walishirikiana na kundi la Kigaidi duniani la Al-Qaeda.

Raisi wa Somalia Hassan Sheikh Mohamed asema Al shabab walishirikiana na Al Qaeda katika kushambulia jengo la kibiashara la Westgate la jijini Nairobi
Raisi wa Somalia Hassan Sheikh Mohamed asema Al shabab walishirikiana na Al Qaeda katika kushambulia jengo la kibiashara la Westgate la jijini Nairobi yahoo.com
Matangazo ya kibiashara

Raisi wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamed akiwa mjini New York kuhudhuria mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa, amesema wanamgambo wa Al-Shabab wameendelea kuwa kitisho cha usalama kwenye nchi yake na nchi jirani na kwamba anatoa pole kwa wananchi wa Kenya kwa kilichotokea.

Kauli ya rais Mohamed, pia iliungwa mkono na waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya Amina Mohamed ambaye amesema tukio hili halikufanywa na wanamgambo wa Al-Shabab peke yao lakini walipata usaidizi toka kwa kundi la Al-Qaeda.

Rais wa Marekani, Barack Obama ameendelea kutoa pole kwa serikali ya Kenya na kuahidi nchi yake kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya usalama vya Kenya kudhibiti makundi ya kigaidi.

Kwa upande wake naibu wa rais wa Kenya, William Ruto ambaye alirejea nyumbani jumatatu usiku akitokea mjini The Hague ambako anaendelea kusikiliza kesi yake na kupewa mapumziko ya juma moja, amelaani tukio hili na kuvipongeza vyombo vya usalama nchini humo kwa kuwadhibiti wanamgambo hao.