MAREKANI-IRAN-UN

Iran na Marekani zaonesha nia ya kuafikiana juu ya mpango wa nyuklia wa Tehran

REUTERS/Eduardo Munoz

Rais wa Marekani Barack Obama na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani kwa pamoja wameonesha nia ya kutafuta suluhu ya kumaliza tofauti zao za kisiasa pamoja na mzozo kuhusu mpango wa taifa hilo kuhusu Nyuklia. Kwenye hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Iran, Hassan Rouhani amesisitiza utayari wa nchi yake kuanza upya mazungumzo na jumuiya ya kimataifa kuhusu mpango wake wa nyuklia licha ya kiongozi huyo kutosema iwapo itaachana na mpango huo.

Matangazo ya kibiashara

Rais Barack Obama alipopata nafasi ya kuzungumza na wanahabari aliwaambia kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Iran na kwamba anamuagiza waziri wake wa mambo ya kigeni John Kerry kuanza mazungumzo na viongozi wa Iran.

Rais Obama pia hakusita kuzungumzia mzozo uliopo kati ya nchi yake na Iran kihistoria jambo ambalo anaamini ndilo limechangia kwa sehemu kubwa nchi ya Iran mara zote kukataa kushirikiana nayo.

Katika hatua nyingine waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amejibu hotuba ya rais wa Iran, na kudai kuwa ni hotuba iliyojaa unafiki na ubinafsi kwa taifa la Iran kwa kuwa rais Rouhan ameshindwa kusema iwapo atasitisha mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni halali na unazingatia haki za msingi za kimataifa msimamo unaopingana na baraza la usalama la umoja wa mataifa linalotaka Iran kuacha urutubishaji wa madini ya uranium.

Makubaliano juu ya mpango huo yamekuwa yakigonga mwamba kwa muda mrefu lakini sasa na Rais mpya wa Iran Hassan Rouhani ameonekana kuonyesha utayari wa kuafikiana juu ya suala hilo.