PAKISTAN

Maafa zaidi yaikumba Pakistani kufuatia tetemeko la ardhi

REUTERS/Sallah Jan

Watu zaidi ya 300 wamepoteza maisha na wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililopiga Kusini Magharibi mwa Pakistani, kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo tetemeko hilo limesababisha madhara makubwa kwa wananchi ambao wengi hawana makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Pakistan imeweka wazi kuwa inaendelea kuhakikisha inatoa msaada kwa waathirika pamoja na kuchukua hatua kuhakikisha wanarejesha hali ya mambo kama ilivyokuwapo hapo awali.

Serikali ya jimbo la Balochistan imetangaza hali ya hatari katika wilaya ya Awaran ambayo imeathiriwa zaidi na tetemeko hilo.

Kwa mujibu wa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa ya nchi hiyo, tetemeko hilo linakadiriwa kuwa nguvu ya 7 nukta 7 ukubwa wa richa.

Jeshi limeendelea na harakati za uokoaji katika eneo hilo ambapo inahofiwa kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka zaidi kutokana na kuhofiwa wamefukiwa katika majengo yaliyoporomoka.

Makundi ya wapiganaji waliojihami kwa silaha yameendelea kuwa changamoto katika wakati huu, siku ya jumanne watu wenye silaha waliripotiwa kuwashambuliwa wahudumu wa afya wanaowahudumia waathirika wa tetemeko hilo.

Tetemeko hilo la ardhi limechangia kuharibiwa kwa huduma za mawasiliano na wasiwasi umeendelea kutanda kwenye majiji mengine kama vile New Delhi na Dubai ambayo yanahofia huenda yakakumbwa na tetemeko kama hilo.