SYRIA-MAREKANI-UN

Marekani yalitaka baraza la usalama la umoja wa mataifa UN kuchukua hatua kali dhidi ya utawala wa Syria

Marekani imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litoe maazimio kuhusu namna ya kumaliza machafuko nchini Syria pamoja na kutangaza hatua kali za kuchukuliwa dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad.

REUTERS/Andrew Burton
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kabla ya kuanza kwa kikao cha 68 cha Umoja huo, Rais wa Marekani Barack Obama ametaka nchi wanachama kutumia mkutano huu kuja na maazimio makali dhidi ya utawala wa Syria, maazimio yatakayotoa hakikisho la usalama nchini humo.

Obama amesema iwapo UN itashindwa kufikia muafaka kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya Syria itakuwa ni aibu kwa dunia na itaonesha chombo hicho kupoteza heshima yake.

Kwa upande wake Rais wa Uturuki, Abdullah Gul, amesema mzozo unaoendelea nchini Syria ni kitisho cha usalama kwa nchi za mashariki ya kati na kwamba lazima suluhisho lipatikane kupitia mkutano huu.

Katika hatua nyingine makundi kadhaa yanayopigana nchini Syria yametangaza kutolitambua Baraza la upinzani la Syria ambalo linasimamia harakati za kuuangusha utawala wa Rais Bashar al-Assad

Azimio hilo limekuja wakati huu ambapo kumeendelea kushuhudiwa mgawanyiko mkubwa kwenye Umoja wao.

Katika taarifa ya pamoja ya makundi ya waasi yenye wafuasi wa dini ya kiislamu wamesema hawatokubali kuwakilishwa na makundi ya upinzani yenye kufungamana na sera za nje ya Taifa lao.

Miongoni mwa makundi yaliyokuja na azimio hilo ni pamoja na Jeshi huru la Syria (Free Syrian Army), Liwa al-Tawhid na Jabhat al-Nusra lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa al-Qaeda.

Aidha katika taarifa hiyo wametaka utekelezaji wa sheria ya kiislamu (sharia) kuzingatiwa.