SYRIA-UN

Wataalamu wa kemikali wa Umoja wa Mataifa UN wawasili nchini Syria kuendelea na uchunguzi

REUTERS/Paulo Filgueiras/UN Photo/Handout via Reuters

Jopo la wataalamu wa maswala ya kemikali wa Umoja wa Mataifa UN limewasili nchini Syria kwa mara nyingine tena kuendelea na uchunguzi katika maeneo yanayodhaniwa kuwa silaha za kemikali zimetumika katika mapigano baina ya vikosi vya serikali na waasi.

Matangazo ya kibiashara

Wataalamu hao wametua katika mji mkuu wa Lebanon Beirut leo asubuhi na baadaye kuelekea Syria wakitumia magari matano ya UN, mashuhuda wa msafara huo wamesema wachunguzi wapatao 8 ndio waliowasili mjini Damascus.

Jopo hilo litachunguza maeneo mengine yanayoshutumiwa kutumia silaha za kemikali kwa takribani mara 14 katika mgogoro huo uliodumu kwa miaka miwili na nusu sasa.
Kiongozi wa jopo hilo Ake Sellstrom amesema anatumaini huenda wakawasilisha ripoti rasmi juu ya uchunguzi wao katikati ya mwezi oktoba.

Septemba 16 Jopo hilo liliwasilisha ripoti iliyobaini kutumika kwa silaha za kemikali nchini humo na kuthibitisha kuwa sumu aina ya sarin ilitumika katika shambulizi la Agosti 21 pembezoni mwa mji wa Damascus na kusababisha mauaji ya mamia ya raia.

Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yamekuwa yakiushutumu utawala wa Rais Bashar al-Assad kuhusika na shambulizi hizo, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Damascus pamoja na mshirika wake Urusi.

Urusi imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa uchunguzi huo haukuwa na uthibitisho kuwa majeshi ya serikali ndiyo yaliyotumia silaha za kemikali katika shambulizi hilo.