Rais Kabila aiomba jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisaidia nchi yake kupata amani
Imechapishwa:
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo DRC, Joseph Kabila amesema kuwa kitendo cha nchi yake kuruhusu wakimbizi kutoka nchini Rwanda kuingia nchini humo ndiko kumechangia kwa sehemu kubwa kushuhudiwa kwa uasi unao onekana sasa.
Rais kabila ametoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye mkutano wa 68 wa Umoja wa mataifa mjini New York, Marekani na kuongeza kuwa wengi wa wakimbizi wa Rwanda waliokimbilia nchini humo wamejiunga na makundi ya waasi ambayo sasa yanapigana na Serikali yake.
Kiongozi huyo ametoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisaidia nchi yake kukabiliana na makundi ya waasi yaliyoko Mashariki mwa nchi hiyo ambayo yameendelea kuwa tishio la usalama wa nchi na raia wa nchi hiyo.
Aidha mashirika ya kijamii Mashariki mwa nchi hiyo yamevitaka vikosi vya Umoja wa mataifa vya kulinda amani MONUSCO vilivyoko nchini humo kuongeza nguvu kuwadhibiti wapiganaji wa makundi ya waasi ambao wanatishia usalama wa rais.