IRAN- MAREKANI

Serikali ya Iran yasema makubaliano kuhusu mpango wake wa Nyuklia huenda yakafikiwa

Rais wa Iran Hassan Rouhan
Rais wa Iran Hassan Rouhan REUTERS/Eduardo Munoz

Serikali ya Iran imesema kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa makubaliano katika kipindi cha mwaka mmoja juu ya mpango wake wa nyuklia unaopingwa na mataifa ya Magharibi tamko lililokuja baada ya kufanyika mazungumzo kati ya waziri wake wa mambo ya nje na mwenzake wa Marekani. 

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo haya ya kwanza kufanyika juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yanakuja baada ya kuchaguliwa kwa rais Hassan Rouhani ambapo waziri wa mambo ya nje Mohammad Javad Zarif amesema makubaliano yatafikiwa.

Marekani kwenye mazungumzo hayo iliwakilishwa na waziri wa mambo ya nje John Kerry ambaye naye akasisitiza umuhimu wa Iran kukubaliana na dunia juu ya kile inachopendekeza kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Umoja wa Ulaya EU ambao umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Iran inashiriki kwenye mazunguzmo ya mpango wake wa nyuklia kupitia mkuu wake wa sera za nje Catherine Ashton ameitaka Tehran ishirikiane na Jumuiya ya Kimataifa.

Rais wa Iran Hassan Rouhani amerejesha tumaini kwa mataifa ya Magharibi baada ya kuonesha utayari wake wa kukaa mezani kujadili mpango wao wa nyuklia ambao wenyewe wanasema una nia njema ya kutengeneza nishati kwa wananchi.