Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali katika maeneo saba nchini Syria
Wataalam wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wanachunguza mashambulizi saba yanayodaiwa kutumia silaha za kemikali na wanatarajia kumaliza kazi yao nchini humo siku ya Jumatatu, Umoja wa Mataifa umesema leo Ijumaa.
Imechapishwa:
Katika taarifa iliyotolewa kutoka mji mkuu wa Syria, ambapo timu hiyo ya wataalamu iliwasili mapema wiki hii, Umoja wa Mataifa umesema wataalam hao wanamatumaini kukamilisha ripoti ya kina ya uchunguzi wao mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Umoja wa Mataifa umejitenga kutoka katika timu ya wakaguzi wa shirika la kuzuia Silaha za Kemikali ambao wanatarajia kuanza kazi ya kuharibu silaha hizo za kemikali nchini Syria juma lijalo.
Mashambulizi yanayodaiwa kutumia silaha za kemikali ambayo yatachunguzwa ni pamoja na shambulizi la Machi 19 huko Khan al-Assal, kaskazini mwa jimbo la Aleppo, ambalo serikali na waasi walitoa taarifa huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kuhusika.
Maeneo mengine ambayo yatachunguzwa ni pamoja na kitongoji cha Sheikh Maqsud katika mji wa Aleppo na Saraqeb Kaskazini Magharibi mwa jimbo la Idlib.
Timu hiyo pia inaendelea kuchunguza shambulizi la Agosti 21 katika eneo la Ghouta nje ya mji wa Damascus, ambalo lilitokea wakati wa kazi ya kwanza ya kundi hilo nchini Syria mwezi uliopita.