KENYA-SOMALIA

Kenya yaapa kutoondoa wanajeshi wake nchini Somalia licha ya vitisho vya Al Shabab

Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku
Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku in2eastafrica.net

Kenya imeapa kutoondoa wanajeshi wake nchini Somalia licha ya vitisho vya mashambulizi zaidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab juma moja baada ya shambulizi kubwa katika jengo la biashara la Westgate jijini Nairobi, lililogharimu maisha ya watu zaidi ya sitini. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa usalama wa ndani Joseph Ole Lenku amewaambia waandishi wa habari kuwa walipeleka wanajeshi wao nchini Somalia kwa kuwa kundi la Al Shabab lilikuwa tishio kwa usalama wa taifa la Kenya na kwamba nchi yake itaendelea kuchukua hatua idi mpaka hapo usalama na matakwa ya nchi hiyo yatakapolindwa.

Mkuu wa kundi la Al Shabab nchini Somalia Ahmed Abdi Godane amesema kuwa shambulizi la Wastgate jijini Nairobi litafuatiwa na mashambulizi mengine ya umwagaji damu zaidi, mpaka hapo Kenya itakapoondoa wanajeshi wake nchini Somalia.

Wakati huo huo jeshi la polisi nchini Kenya limesema kuwa linawashikilia washukiwa 8 wanaokisiwa kuhusika na shambulizi la kigaidi la siku ya Jumamosi ambapo washukiwa wengine watatu wameachiwa baada ya kuithibitishia polisi kutokuhusika.