SUDANI

Rais Omar al-Bashir ahimizwa kuahirisha mpango wa kubana matumizi uliozusha machafuko

Makundi ya kiislamu na wanachama wa chama tawala nchini Sudani wamemtaka Rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir kuahirisha mpango wa kubana matumizi uliopitishwa na serikali yake ili kutuliza jazba za wananchi wanaoandamana kwa takribani juma moja sasa.

Matangazo ya kibiashara

Wanachama 31 wa makundi ya kiislamu na wale wa chama tawala cha NCP wametia saini nakala ya mapendekezo ya kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka, hatua ambayo ni ya kwanza kufanyika ndani ya utawala wa Bashir tangu kuanza kwa machafuko hayo.

Wito huo unakuja baada ya polisi kushutumiwa na wanaharakati na makundi ya kutetea haki za binadamu kutumia silaha za moto dhidi ya waandamanaji mjini Khartoum.

Watu kadhaa wamejeruhiwa siku ya jumamosi baada ya polisi kuwashambuliwa waombolezaji waliokuwa katika mazishi ya mtu mmoja aliyeuawa katika maandamano yanayoendelea nchini humo.

Mabomu ya kutoa machozi yalirushwa kuwatawanya maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya mhudumu wa afya Salah al-Sanhouri aliyeuawa siku ya ijumaa.

Maandamano hayo yanaingia katika siku ya saba hii leo na inaelezwa kuwa tayari watu zaidi ya sitini wamepoteza maisha katika machafuko hayo ya kuipinga serikali iliyoondoa ruzuku katika mafuta.