NIGERIA

Kundi la Wanamgambo la Boko Haram limewaua wanafunzi wapatao 50 wa Chuo Cha Kilimo nchini Nigeria

Kundi la Wanamgambo wa Kiislam la Boko Haram la nchini Nigeria limeendelea kuwa kitisho kwa usalama wa nchi hiyo kufuatia kuwaua kinyama wanafunzi wanaofikia hamsini kwenye shambulizi baya la hivi karibuni lililotekelezwa kwenye Mji wa Gujba kwenye Jimbo la Yobe.

Chuo Cha Kilimo huko Yobe nchini Nigeria kikiwa kimeshambuliwa na Wanamgambo wa Kundi la Boko Haram
Chuo Cha Kilimo huko Yobe nchini Nigeria kikiwa kimeshambuliwa na Wanamgambo wa Kundi la Boko Haram
Matangazo ya kibiashara

Wafuasi wa Kundi la Wanamgambo wa Boko Haram wanatajwa kuvamia Chuo Cha Kilimo na kisha kufyatua risasi kwa wanafunzi waliokuwa wanaendelea na masomo yao kwenye eneo la Chuo hicho kitu ambacho kimezidisha hofu ya wananchi wa Nigeria kwenye majimbo kadhaa.

Msemaji wa Jeshi nchini Nigeria katika Jimbo la Yobe Lazarus Eli amethibitisha wafuasi wa Kundi la Wanamgambo wa Boko Haram wakiwa wamejihamia na silaha nzito za kivita kuvamia Chuo Cha Kilimo kisha wakaanza kufyatua risasi kuwalenga wanafunzi hao.

Eli amesisitiza Wanamgambo wa Boko Haram walikwenda katika Chuo hicho wakiwa na silaha pamoja na vilipuzi kuhakikisha mpango wao unafanikiwa kama ambavyo waliupanga na kufanikiwa kuwaua wanafunzi hao arobaini na kuwaacha wengine wanne wakijeruhiwa.

Jeshi limethubutu kuita shambulizi hilo la Kundi la Wanamgambo la Boko Haram kuwa ni la kigaidi na linaonekana lilipangwa kwa kipindi kirefu kabla ya kutekelezwa na kuendelea vitendo vyao vya kinyama katika Majimbo ya nchi hiyo.

Salamu Ibrahim ni mmoja wa wanafunzi walionusurika kwenye shambulizi hilo la kigaidi lililotekelezwa na Kundi la Wanamgambo la Boko Haram na kusema aliwaona wakipita sehemu wanazolala wanafunzi na kuendelea kufyatua risasi kwa kila waliyekutana naye.

Shambulizi hili limelaaniwa vikali mno na Mataifa ya Magharibi na kusema linadhihirisha Kundi la Wanamgambo la Boko Haram limekuwa na msimamo mkali juu ya kupinga kuenea kwa eleimu ya magharibi wanayoipinga kwa kiwango kikubwa.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton ameliita shambulizi hilo kuwa la kinyama na linapaswa kulaaniwa vikali na juhudi za haraka zinahitajika katika kuhakikisha matukio kama hayo yanadhibitiwa katika siku za usoni.

Kundi la Wanamgambo la Boko Haram limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha elimu kutoka mataifa ya magharibi haienei katika nchi hiyo huku wakisisitiza ni lazima eneo la Kaskazini liwe chini ya Sharia za Kiislam.

Mnamo mwezi Julai katika Mji wa Mamudo uliopo kwenye Jimbo la Yobe ulishuhudia vifo vya wanafunzi arobaini na moja baada ya Kundi la Wanamgambo la Boko Haram kufanya shambulizi kulenga shule moja.