Marekani imesisitiza suluhu juu ya mpango wa nyuklia wa Iran itapatikana katika kipindi cha miezi sita ijayo
Marekani imeendelea kuwa na matumaini ya kwamba suluhu juu ya mpango wa nyuklia unaotekelezwa na Serikali ya Iran utafanikiwa katika kipindi cha miesi sita ijayo iwapo tu Serikali ya Tehran itakuwa na nia ya dhati kutoa ushirikiano kwenye hilo.
Imechapishwa:
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema kumekuwa na ishara zinazodhihirisha mpango huo unaweza ukafikia suluhu mapema kutokana na Rais wa Iran Hassan Rouhani kuonesha utayari wake wa kutoa ushirikiano wa dhati.
Kerry amesema kuna uwezekano muafaka ukafikiwa mapema kutokana na Iran kuonesha utayari wa kuhakikisha suluhu inafikiwa kitu ambacho kitasaidia pande zote zinazoshiriki kwenye mkakati huo ziwe na kazi rahisi mbele yao.
Waziri Kerry amesema huu ni wakati wa kuhakikisha muafaka wa kweli unafikiwa na kama hilo litafanyika basi litasaidia kwa kiwango kikubwa kuhakikisha dunia inajiepusha na hatari ya uwepo wa silaha za maangamizi.
Kiongozi huo mwenye dhamana ya masuala ya mambo ya nje amesema iwapo suala hilo litafanyika kwa amani ni wazi kabisa litaonekana na hivyo dunia itajua kwa wazi kilichokuwa kinafanywa na Iran na hivyo mahusiano yao na dunia yatakuwa mazuri.
Marekani imetangaza utayari wake wa kuondoa vikwazo vyote kwa nchi ya Iran vikiwemo vile vya kibiashara iwapo tu nchi hiyo itakuwa na nia ya dhati katika kufanya mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia.
Waziri Kerry amesema wanachotaka kukifanya kwa sasa ni kuhakikisha wanafanya uchunguzi kubaini hatua ambazo zimepingwa na Irana kwenye mpango wa nyuklia na kama walifanikiwa kutengeneza mabomu.
Rais wa Iran Rouhani alijitokeza kabla ya Mkutano Mkuu wa Sirini na Nane wa Umoja wa Mataifa UNGA na kuweka bayana utayari wa nchi yake kushirikiana na mataifa mengine juu ya mpango wake nyuklia.
Iran imekuwa ikikataa pendekezo la kuacha kurutubisha nyuklia kwani yenyewe imekuwa ikisema inatekeleza mpango huo kwa lengo jema kabisa la kuhakikisha wanazalisha nishati ya umeme ya uhakika itakayotumiwa na wananchi wao na si kuzalisha mabomu kama inavyotuhumiwa na Mataifa ya Magharibi.