SYRIA-UN

Serikali ya Syria yatangaza utayari wake wa kushirikiana na Umoja wa Mataifa UN juu ya azimio la kuteketeza silaha zake za kemikali

Rais wa Syria Bashar Al Assad ambaye ametangaza utayari wa nchi yake kutoa ushirikiano kwa Umoja wa Mataifa UN juu ya kutetekeza silaha zake za kemikali
Rais wa Syria Bashar Al Assad ambaye ametangaza utayari wa nchi yake kutoa ushirikiano kwa Umoja wa Mataifa UN juu ya kutetekeza silaha zake za kemikali REUTERS/SANA/Handout via Reuters

Serikali ya Syria imesema ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Umoja wa Mataifa UN katika kuhakikisha azimio lililopitishwa juma lililopita la kutaka kuangamiza silaha za kemikali wanazozimiliki linafanikiwa na kutekelezwa kwa namna ambavyo Umoja huo inaona ni sahihi.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Syria chini ya rais Bashar Al Assad imesema itafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha azimio hilo linatekelezwa iapsavyo na wapo tayari kuwapokea Waatalam wa Masuala ya Silaha za kemikali ambao wanaelekea Damascus kuanza kazi hiyo.

Rais Assad amesema watashirikiana na Umoja wa Mataifa UN ili kuhakikisha azimio hilo linafanywa kazi kutokana na wao kuwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya silaha za kemikali ndani ya mipaka yake kwa kuwa wanafahamu madhara yake ni makubwa kwa wananchi.

Serikali ya Syria imesema hakuna sababu yoyote kwa wao kuzuia kufanyika kwa shughuli hiyo ya kuangamiza silaha za kemikali wanazozimiliki kutokana na kuonekana ni hatari kwa usalama wa wananchi wake.

Kauli ya Serikali inakuja ikiwa ni majuma mawili tangu Rais Assad aweke bayana suala la kuangamiza silaha za kemikali wanazozimiliki litachukua zaidi ya mwaka mmoja sanjari na gharama zake ambazo ni dola za Marekani bilioni moja.

Haya yanakuja huku Wataalam ishirini wa Masuala ya Silaha za Kemikali wakitarajiwa kuwasili Damascus kwa ajili ya kuanza kuangalia namna amnavyo itafanyika ili kuhakikisha silaha hizo zote zinateketezwa haraka iwezekanavyo.

Kazi ya kwanza ya wataalam hao itakuwa ni kufanya uchunguzi na kubaini maeneo yote ambayo silaha hizi zimehifadhiwa ikiwa ni pamoja na idadi yake kabla hawajatoa ushauri wa namna nzuri ya kuhakikisha silaha hizo zote zinaangamizwa kwa wakati.

Zoezi hili linaendelea kipindi hiki kumekuwa na juhudi za kuhakikisha pande zinazohasimiana kwenye mgogoro wa Syria zinarejea kwenye meza ya mazungumzo ili kusaka suluhu kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia nguvu za kijeshi.

Kiongozi wa Upinzani Ahmad Jarba alikutana kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambapo alimhakikishia watapeleka ujumbe wao kwenye mazungumzo ya Geneva.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Muallem amesisitiza kuwa wataenda kwenye mazungumzo ya Geneva lakini hakuna sharti linalomtaka Rais Assad aondokea madarakani ndiyo majadiliano hayo yafanyike.